RUGE WA ESCROW USIPIME! - LEKULE

Breaking

6 May 2015

RUGE WA ESCROW USIPIME!


LOOH usipime! Yule bilionea aliyezidi kupata jina kwa kutajwa kwenye sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, James Rugemalira ‘Ruge wa Escrow’, amefanya maadhimisho makubwa aliyoyaita kumbukumbu ya kifo cha mjukuu wake, Isabella Benita Bulengo.

James Rugemalira ‘Ruge wa Escrow’.

Kumbukumbu hiyo ya kuadhimisha miaka mitatu tangu kifo, ilifanyika Aprili 25, mwaka huu nyumbani kwa Bilionea Ruge, Makongo Juu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu kibao, wakubwa kwa wadogo.

KIFO CHA MJUKUU
Isabella alifariki dunia Aprili 24, 2012 akiwa na umri wa miaka 5 kwa ugonjwa ambao haukutajwa na kuzikwa Aprili 28 kwenye kaburi lililopo ndani ya nyumba ya bilionea huyo.

WATU WALISHANGAA KABURI
Baadhi ya waalikwa kwenye kumbukumbu hiyo walishangazwa na kitendo cha kaburi la mjukuu huyo kujengwa ndani ya ua na kunakshiwa kwa urembo wa kuvutia huku ukutani kukiwa na msalaba wa kudumu.
Mbali na kaburi la mjukuu huyo lililofunikwa maua na mishumaa kwa pembeni, pia ndani humo kuna kaburi lingine linalodaiwa kuwa ni la mama wa Ruge.
Siku hiyo mama wa marehemu Isabella aitwaye Evelyne James alikuwepo, mke wa Ruge naye alikuwepo huku Ruge mwenyewe akiwa amevaa ‘full nyeupe’ alining’iniza msalaba shingoni.

KUMBUKUMBU ILIANZA HIVI
Maadhimisho hayo yalianza kwa misa nyumbani hapo huku wanandugu wakishiriki kumkumbuka marehemu kwa kuweka maua kwenye kaburi.

UKAFUATA MUDA WA CHAKULA
Baada ya misa ndipo muda wa maakuli ukawadia huku buffet za kutosha zikiwa kila upande, waalikwa walikula wakasaza.
“Jamani kuna watu wanajua kuandaa shughuli. Mimi nilikwenda nikijua ni kitu kidogo cha mara moja na kuondoka lakini kufika looh! Makubwa! Chakula cha kumwaga, minyamanyama, mikuku, ng’ombe mpaka samaki, yaani mazagazaga yote,” alisema mwalikwa mmoja.

MUDA WA ’MAMBO YETU’ SASA
Baada ya vyakula, ukafuata muda wa vinywaji mbalimbali, zikiwemo pombe ‘mambo yetu’ ambapo meza zilichafuka kwa chupa na milio yake.
“Vinywaji vilikuwepo aisee! Wenye kunywa bia sawa, wa soda haya, wa juisi twende kazi! Yaani, we acha tu!” alisema mwalikwa huyo kwa jinsi alivyoishuhudia shughuli hiyo.

MAKADIRIO YA BAJETI
Ingawa si rahisi kujua bajeti ya fedha iliyotumika lakini mwalikwa mmoja alisema kwa macho ya haraka, huenda shilingi milioni ishirini (20,000,000) zilitumbukia kwenye kumbukumbu hiyo.

BURUDANI ZILIZOPAMBA
Kama hiyo haitoshi, kumbukumbu hiyo pia ilipambwa kwa nyimbo mbalimbali za kabila la Kihaya na mwishowe kumaliziwa na muziki wa Bongo Fleva ambapo ndugu na waalikwa mbalimbali waliongozwa na Ruge mwenyewe aliyeingia kwenye ‘dansing floo’ kucheza kiasi kwamba kwa mtu ambaye alikuwa nje ya nyumba hiyo asingejua kuwa ile haikuwa sherehe.

SAA 7 USIKU, MAMBO BADO
Mpaka chanzo chetu kinaondoka eneo la tukio saa saba usiku, muziki ulikuwa ukiendelea kuchezwa huku baadhi ya watu waliokuwa wakisakata muziki huo wakitokwa jasho jembamba kama siyo jepesi!

KWA NINI RUGE WA ESCROW?
Akaunti ya Tegeta Escrow ilimpa jina kubwa Ruge kufuatia malipo ya mabilioni ya shilingi aliyolipwa kupitia kampuni yake ya VIP Engineering iliyokuwa ikifanya kazi na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa kufua umeme na kuuza Tanesco. Ruge alilipwa pesa hizo baada ya kampuni yake kujitoa ushirika na IPTL.
Baada ya hapo, skendo iliibuka, ikibainika kuwa, ndani ya fedha hizo na yeye Ruge kupitia Benki ya Mkombozi ya Dar ‘aliwakatia’ mshiko baadhi ya watu, wakiwemo watumishi wa serikali na viongozi wa dini bila kujulikana aliwapa kwa ajili ya nini.

Sakata la Escrow likaibua mjadala mkubwa bungeni mjini Dodoma, watu wakaguswa miongoni mwao ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sylvester Muhongo, naibu wake, Steven Masele, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Wengine ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini (kabla ya Muhongo), William Ngeleja, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka na baadhi ya watumishi wa serikali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Sherehe hiyo ya kumbukumbu ya mjukuu wake, ilifanyika siku tatu tu tangu afanye sherehe ya kukata na shoka ya kufurahia siku yake (Ruge) ya kuzaliwa.

No comments: