Maji ya mvua yenye kasi yakitapakaa kila eneo la Zanzibar.
Wananchi wakihangaika kwenye mafuriko kutokana na mvua
Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar nako kumefurika.
Na Abdulla Ali wa Maelezo, Zanzibar
Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Visiwani Zanzibar zimesababisha hasara kubwa ikiwemo upotevu mali na mifugo, uharibifu wa miundombinu pamoja na kusababisha vifo vya watu.
Hadi sasa watu wawili ambao ni Nd. Juma Hamad (25) mkaazi wa Mwanakwerekwe na mtoto mmoja mkaazi wa Kinuni anaekisiwa kuwa na miaka 8 wamepoteza maisha. Wote wawili ni kutoka Wilaya ya Magharibi Unguja.
Hayo yamweelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na athari za mvua hizo katika ukumbi wa Karume House, Mjini Zanzibar.
Amesema mvua hizo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea athari kubwa katika maeneo hayo ikiwemo vifo vya watu, uharibifu wa nyumba za makaazi na upotevu wa mali na mifugo.
Aidha Waziri Aboud amesema kuwa maiti ya mtoto imeshapatikana na kuzikwa jana Tarehe 3/5/2015 na maiti ya Nd. Juma Hamad bado haijapatikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Amefahamisha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo ni pamoja na Magomeni, Jang'ombe, Nyerere, Sebleni, Sogea, Mwanakwerekwe, Welezo, Kisauni, Tomondo, Mombasa, Kinuni, Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae, Bububu na Kwaalinato, ambapo maeneo yote hayo yanapatikana ndani ya Mkoa wa Mijini Magharibi.
Ametanabahisha kuwa, kwa vile mvua bado zinaendelea kunyesha ni vyema wananchi wakachukua tahadhari ili kujiepusha na athari zaidi zinazoweza kujitokeza, ikiwemo wazazi kuangalia watoto wao na kuhakikisha hawachezi karibu na maeneo yanayotuama maji, kwa wale wanaoishi mabondeni ni vyema wakahama sehemu hizo.
Waziri Aboud pia amewataka wananchi waliochimba mashimo katika maeneo ya makaazi wawe waangalifu kwa kuyafunika haraka iwezekanavyo , kuchemsha maji wanayoyatumia, kuhifadhi chakula ili kuepukana na maradhi ya miripuko pamoja na kufuata kanuni za afya ikiwemo usafi binafsi na maeneo yanayowazunguka.
Vilevile amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwani Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa hali ya maisha kwa wananchi hao inarudi kama kawaida pamoja na kuwapa pole wale wote waliopoteza jamaa na mali zao.
No comments:
Post a Comment