Mtwara yasimama saa 24 .....Huduma zafungwa kukumbuka waliouawa wakati wa vurugu za gesi - LEKULE

Breaking

23 May 2015

Mtwara yasimama saa 24 .....Huduma zafungwa kukumbuka waliouawa wakati wa vurugu za gesi

HUDUMA  za kijamii mkoani Mtwara jana zilisimama kutokana na baadhi ya wananchi kudai kuwa wanaomboleza vifo vya watu vilivyotokea wakati wa vurugu za gesi hivyo kupelekea huduma za kijamii kusimama.
 
Mmoja wa wananchi walioathiriwa na mgomo huo, Hilal John aliyekuwa safarini kuelekea Newala lakini alikosa usafiri kutokana na kumbukumbu hiyo alisema hatua hiyo imeathiri wananchi wa hali ya chini.
 
Alisema hali hiyo imesababisha wasafiri wanaokwenda wilaya zote pamoja na baadhi ya mikoa kushindwa kuondoka  kutokana na kutokuwepo kwa huduma hiyo kwa siku nzima ya jana.
 
Si hivyo tu, maduka mbalimbali nayo yalifungwa na hivyo kusababisha baadhi ya watu kukosa huduma hizo.
 
“Nimi nilikuwa naelekea Newala kwenye usaili lakini nimeshindwa kwenda hadi muda huu niko kituoni hakuna hata dalili ya magari zaidi ya mabasi ya kwenda Dar es salaam ndio yapo, hii inatufanya tushindwe kuelewa kwanini huu mgomo unafikia hatua ya kusimamisha safari  na huduma muhimu za kijamii”  alihoji John
 
Kwa upande wake Fatuma Halfani anayemiliki mgahawa katika kituo cha mabasi alisema mgomo huo kwa sehemu kubwa umeathiri akina mama lishe ambao wamekuwa wakitegemea biashara hiyo kuendeshea maisha yao.
 
 Alisema amekuwa akifanya biashara hiyo kwa muda lakini analazimika kupata hasara kutokana na mgomo ulipo ili kuepuka vurugu  .
 
Halfan alisema kitendo cha wananchi kuweka maombolezo ya mgomo kwa huduma za kijamii ambazo ni muhimu zinazowagusa wananchi wa hali ya chini ni jambo la kusikitisha kwa kuwa wananchi wa hali ya juu wanaendelea kupata  huduma hizo.
Naye Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Mtwara George Salala alisema Mtwara ipo katika hali ya utulivu hivyo kuwataka wananchi kuendeleza amani iliyopo na kuwaonya wachache ambao watajaribu kufanya vurugu ambazo zitasababisha uvunjifu wa amani.
 
Alisema Jeshi la polisi linawataka waliokata leseni kwaajili ya biashara wafanye biashara na kwa watoa huduma sokoni wafungue maduka kwa kuwa hawatakusudia kuwachokoza kwa kuwa wao ni serikali na zaidi ofisi zote za serikali zilikuwa zikifanya kazi kama kawaida.
 

 “Sisi kama jeshi la polisi hatuko tayari kuona watu wanaingilia uhuru wa watu wengine hatutasita kuwachukulia hatua na kuwafikisha mbele ya sheria tunaitaka jamii ione madai hayo kama hayana tija ili tuweze kusonga mbele lakini hatuwezi kusonga mbele”  alisema Salala

No comments: