Mrema Ataka Rais Kikwete Aongeze Muda Wa Kuwa Rais ili Akamilishe Mchakato wa Katiba Inayopendekezwa - LEKULE

Breaking

4 May 2015

Mrema Ataka Rais Kikwete Aongeze Muda Wa Kuwa Rais ili Akamilishe Mchakato wa Katiba Inayopendekezwa


Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amesema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa kuongoza nchi kwa muda ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura. 
 
Hivi karibuni viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walidai kuwa Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC) inachelewesha uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa lengo la kutaka kumwongezea Rais Kikwete muda wa kukaa Ikulu.
 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ni miezi mitatu imebaki kabla ya kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa ratiba, majimbo yaliyogawanywa, watumishi wala vituo vya uchaguzi bado haviwekwa bayana na wala haifahamiki kazi ya uandikishaji katika Daftari la Wapigakura halijakamilika katika mikoa miwili.
 
“Hiyo ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe.
 
Akizungumza na mtandao  huu jana, Mrema alisema yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kutoa wazo la kutaka Rais Kikwete aongezewe muda zaidi wa kukaa Ikulu kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo ni ya muhimu kwa Taifa yanayotakiwa kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu.
 
Mrema alisema alitoa maoni hayo mwaka jana wakati viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) walipokutana na Rais Kikwete mjini Dodoma, lakini alishangaa kuona viongozi wengine wakipinga wazo hilo.
 
“Nilitoa ushauri Rais Kikwete akiwepo. Nilisema tusogeze Uchaguzi Mkuu mbele kwa miaka miwili ili atuachie nchi ikiwa salama, lakini wapinzani wamejiandaa kuingia Ikulu waliniona mimi kama bundi,” alisema Mrema.
 
Aliongeza kuwa hata Rais Kikwete hakuonekana kufurahishwa na hali hiyo iliyojitokeza baada ya kauli yake na kwamba, hivi sasa amebaini kuwa kiongozi huyo wa nchi hataki kuongezewa hata siku moja ya kuendelea kukaa Ikulu.
 
“Sema kwa sababu wenzangu wamejiandaa kuingia Ikulu mwaka huu, wameshawaandaa hata wake zao kuwa ‘ma-first lady’, lakini ukweli ni kwamba hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa lazima kuwe na muda wa mpito.
 
“Simfanyii mtu kampeni, ninachosema ni kwamba, mambo hayajakamilika na tunataka yakamilike na michakato yote aliyeianzisha ni Rais Kikwete, ni vyema akaimaliza,” alisema Mrema.
 
Akihutubia kwenye sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jijini Mwanza juzi, Rais Kikwete alisema hana mpango wa kuongeza muda kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
 
“Nawashangaa wanaodai kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza muda wa urais, sina mpango wa kufanya hivyo, tarehe imepangwa na uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa Katiba,” alisema Rais Kikwete.

No comments: