Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba
amesema kupungua kwa umaskini kunakoelezwa na baadhi ya wataalamu na
wasomi ni suala la kitakwimu ambalo ni gumu kulithibitisha.
Aliyasema
hayo jana, Msasani, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuaga mwili wa
John Nyerere. Mtoto huyo wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, alifariki
dunia Mei 9, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na
anasafirishwa leo kwenda Butiama kwa maziko.
Alisema
ugumu wa maisha umeongezeka na akafafanua kuwa licha ya taarifa
zinazotolewa na wataalamu kwamba uchumi umekua ni vyema kila mmoja
akajitathmini kuanzia ngazi ya kaya kwani huko ndiko hali halisi iliko.
“Mimi
katika kaya yangu bado hatujaendelea. Maendeleo hayajafika kwa kiwango
cha kumudu gharama zote kwa kila mmoja wetu. Hatuhitaji kuambiwa juu ya
maendeleo yetu kwa kutumia taarifa za kisomi ambazo mara nyingi ni
wastani. Angalia familia yako ikoje,” alisema Mramba.
Kauli
ya Mramba imekuja siku chache baada ya Benki ya Dunia (WB) kuzindua
ripoti yake juu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania, mapema mwezi huu,
ambayo inabainisha kuwa katika kipindi kati ya 2007 mpaka 2012, umaskini
umepungua kwa asilimia 70 jijini Dar hapa huku ukishuka kwa asilimia 15
mikoani.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa katika kipindi hicho, umaskini unapungua kwa asilimia moja kila mwaka.
Pia,
alielezea kuporomoka kwa shilingi na kubainisha kuwa ni moja ya sababu
zinazochangia ugumu wa maisha kwa Watanzania maskini na kueleza kuwa ni
jambo linalotaka mikakati makini kukabiliana nalo.
“Dola
moja ya Marekani imewahi kuwa sawa na Sh7. Kiasi hicho cha fedha
kilikuwa kinaweza kununua mbuzi wakati huo lakini dola hiyo hivi sasa ni
Sh2,000. Hebu niambie kiasi hicho kinanunua nini wakati huu?” alihoji
Mramba.
Wakati huo huo, familia ya Baba wa Taifa,
imelishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa msaada ilioutoa
katika kipindi chote cha kumuuguza hadi kufariki kwa ndugu yao.
Shukrani
hizo zilitolewa na mdogo wa marehemu, Makongoro Nyerere alipokuwa
akisoma wasifu wa marehemu mbele ya Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib
Bilal na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Makongoro
alimaliza kusoma wasifu huo kwa taabu kwani alishikwa na majonzi kiasi
cha kulia kwa kwikwi na kuwahuzunisha mamia ya waombolezaji msibani
hapo.
Aidha, Mbunge wa Monduli, Edward Lowasa ametuma
salamu za rambirambi za kumfariji Mama Maria Nyerere na familia ya Baba
wa Taifa.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
kifo cha John Nyerere, mtoto wa mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius
Nyerere. Kifo chake kimetonesha kidonda siyo kwa familia tu, bali kwa
Watanzania wote, kidonda cha kifo cha Mwalimu ambacho bado ni kibichi
miaka 16 baada ya kifo chake,” alisema Lowasa
No comments:
Post a Comment