CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kumpata mgombea wake wa urais Agosti 4, mwaka huu.
Kupatikana kwa mgombea huyo kutatokana na uamuzi wa mkutano mkuu wa taifa, ambacho ndio chombo cha juu cha uamuzi.
Kauli
hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, wakati akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa kikao
cha Kamati Kuu kilichoketi kwa siku mbili.
Alisema
pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili ratiba ya kuwapata
wagombea wa udiwani, ubunge na urais ambao utaratibu wa kuwapata utaanza
Mei 18 hadi Agosti 4.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ngazi ya udiwani utaanza Mei 28 hadi Juni 25.
“Julai
Mosi hadi 10 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu kwa kata ambazo tuna
madiwani na Julai 15 hadi 20 utakuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea
udiwani wa kata pamoja na wale wa viti maalumu.
“Mei
18, hadi Juni 25 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu za ubunge kwa
majimbo ambayo hatuna wabunge kwa sasa pamoja na viti maalumu, na Julai 6
hadi 10 ni uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge kwa majimbo ambayo
tuna wabunge kwa sasa.
“…
Julai 20 hadi 25 ni uteuzi wa awali kwa wagombea ubunge kazi
itakayofanywa na Kamati tendaji za majimbo. Hata hivyo pia Julai 20 hadi
25 ni kuchukua na kurejesha fomu za mgombea urais ambazo zitasimamiwa
na Makao Makuu,” ilionyesha ratiba hiyo iliyotolewa na Chadema.
Pamoja
na mchakato huo, Chadema imesema kuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea
ubunge utafanyika Agosti 1-2 kazi ambayo itafanywa na Kamati Kuu ya
chama hicho.
“Agosti
3, mwaka huu kitaketi kikao cha Baraza Kuu chini ya utaratibu wa Kamati
Kuu na Agosti 4 utafanyika Mkutano Mkuu wa Taifa ambao utafanya kazi ya
kuchagua mgombea urais kwa mujibu wa Katiba ya Chadema,” alisema Mbowe.
Akizungumzia
kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, Mbowe alisema wamepokea,
kujadili na kukubaliana makubalino yaliyokwishafikiwa na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa
– umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana ukiwa ni kikundi shinikizi
katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za Bunge Maalumu la
Katiba, inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Kuhusu
Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema wamebaini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
na Serikali hawana dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya
kutosha yakiwamo matakwa ya kisheria, kitaalamu na kibajeti ili
kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa Katiba.
Kuhusu
kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema baada ya kujadili kwa
kina wamebaini kuna haja kura hiyo isogezwe mbele hadi baada ya
kumalizika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumzia
kuhusu uwapo wa Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema kimsingi Chadema imebaini
kutokuwapo kwa maandalizi ya vifaa, fedha, kutangaza majimbo, kata mpya
pamoja na vituo.
“Kamati
Kuu imeazimia kuiomba Serikali kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika
Oktoba kwa mujibu wa Katiba na Serikali ya CCM isijiandae kutumia
kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi sio jambo la dharura
bali limekuwa likijulikana tangu miaka mitano iliyopita,” alisema.
Wakati
Chadema wakitangaza ratiba yao ya kuwapata wagombea katika majimbo,
vyama wenza vinavyounda Ukawa vya CUF na NCCR-Mageuzi vilishatangaza
ratiba zao, lakini hadi sasa vimekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa
ndani wa kuwapata wagombea wao.
No comments:
Post a Comment