Bujumbura. Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe juzi alikutana na Rais wa
Burundi, Pierre Nkurunziza na kumwachia maswali manne atakayoyajibu
katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
kilichoitishwa na Rais Jakaya Kikwete ili kuokoa hali ya machafuko
yanayohofiwa kutokea Burundi.
Kikao hicho kinatarajiwa
kufanyika Dar es Salaam, Mei 13, mwaka huu na kuhudhuriwa na marais wa
jumuiya hiyo, kitajadili hali ya kisiasa Burundi.
Hofu
ya machafuko imejitokeza baada ya Rais Nkurunziza kutaka kugombea tena
katika uchaguzi ujao, jambo linalopingwa na vyama vya upinzani na
wanaharakati nchini humo.
Juzi, Waziri Membe
aliwaongoza mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Amina Mohammed na
Rwanda, Louise Mushikiwabo kuzungumza na Rais Nkurunziza ili kujua ni
jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Maswali hayo ni kuhusu uchaguzi ujao kama utakuwa wa haki, amani, huru na endapo nchi itatawalika baada ya uchaguzi huo.
“Hatupendi vurugu na ndiyo maana tunataka kukutana kutatua tatizo lililopo,” alisema.
Tangu
chama tawala cha nchi hiyo CNDD-FDD kimpitishe Rais Nkurunziza kuwania
nafasi hiyo, maandamano ya kupinga uteuzi wake yalianza jijini
Bujumbura.
Hivi sasa mitaa ya Bujumbura iko kimya, huku
shughuli zote za kibiashara zikiwa zimesitishwa kutokana na polisi
kuzuia mikusanyiko ya watu.
No comments:
Post a Comment