BAADHI ya madereva waliogoma katika mgomo wa juzi uliodumu kwa siku mbili wameanza kufukuzwa kazi na wamiliki wa mabasi hayo.
Mhasibu
Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania(UWAMATA) Issa Regan aliwataka
matajiri kuwarudisha kazini dereva huyo na kama hawatawarudisha
watawaambia madereva wote wa kampuni hiyo kugoma.
Regan
aliongeza kuwa makosa sio ya madereva hao kwa kuwa walitii umoja huo na
viongozi wao ndio waliwaambia kugoma hivyo kumfuza dereva sio sawa.
“Nasikitika
kwa kitendo hicho na kama hawa matajiri wanataka vita basi tupo radhi
kufanya hivyo lakini sisi tunataka kujenga mahusiano mazuri kati ya
madereva na mabosi wao suala letu lilikuwa ni suala la msingi mtu
ashindwe kuelewa mi sijui wanatutaka nini” alisema Regani.
Alimtaja dereva aliyefukuzwa na mmiliki wake kuwa ni Seif Kitumbo wa basi la kwenda Musoma, ambaye ni wa kampuni ya Osaka.
Regan
alieleza kuwa wameshatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama kuwa endapo
akipotea kiongozi yeyote wa chama chetu cha madereva bila mawasiliano
(kutekwa) sisi tutashughulika na matajiri.
Naye
dereva aliyefukuzwa katika gari hilo kwa sababu ya mgomo, Kitumbo
alisema kuwa chanzo cha yeye kufukuzwa ni kwa sababu aligoma na tajiri
wake alimwambia kuwa amemsababishia hasara.
“Nimekuja
kwenye chama chetu hiki ili niweze kusaidiwa nimefanya kazi kwa muda wa
mwaka mmoja na miezi 11 sijawahi kusababisha ajali yoyote”alisema Kitumbo.
Naye
Katibu Mkuu wa UWAMATA,Abdala Lubala alisema athari za kutoajiriwa
ndizo hizo kama Kitumbo angekuwa anamkataba asingefukuzwa kirahisi kama
hivyo.
“Wamiliki
wanatutafuta sisi tuligoma kwa haki yetu madereva tutafata sheria za
kuweza kumsaidia huyu dereva arudishwe kazini lakini dunia imekubali
madai yetu kuwa ni ya msingi”alisema Lubala.
Amri ya Kurudi Shule Yafutwa
Akizungumza
na waandishi wa habari jana kituoni hapo, Katibu wa Umoja huo Abdul
Lubanda alisema kero moja kati ya madai yao tayari limefanyiwa kazi na
Serikali.
Alisema kero hiyo ni ile ya madereva kurudi shule kusoma kila baada ya miaka mitatu ambayo walikuwa wakiipinga.
“Baada
ya kikao cha jana (juzi)tuliondoka na Mkuu wa Wilaya, Paul Makonda hadi
kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kushughulikia masuala ambayo tulikuwa
tunayalalamikia pamoja na kujua tume iliyoundwa.
“Tulikuwa
pia na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta tulikuta tayari kero ya kurudi
shule imeondolewa kimaandishi kama ambavyo tuliomba,” alisema.
Alisema
walielezwa muundo wa tume (kamati) iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda kwamba itajumuisha makatibu wakuu wa wizara nne pamoja na taasisi
mbalimbali zinazohusiana na mambo ya usafirishaji.
Alitaja
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi, Kazi na Ajira na Miundombinu
na vyama hivyo ni Chama Cha Wamiliki wa Malori (TATOA), Chama cha
Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (SUMATRA), Chama cha Madereva, Chama cha Kutetea Abiria
(CHAKUA).
Alisema
kamati hiyo itakuwa ikikutana mara moja kila mwezi na kwamba
ital;azimika kukutana mara kwa mara iwapo kuna tatizo kama
lililojitokeza hivi sasa la mgomo ili kulipatia ufumbuzi.
“Chama
cha Madereva tumepatiwa nafasi tano za wajumbe ndani ya kamati hiyo leo
(jana) tumekuwatana ili kuwateua wawakilishi wetu, kamati itakapoanza
kazi itashughulikia suala la mikataba ndani ya siku 30, tunataka kila
dereva apatiwe mkataba bora na si bora mkataba na mwajiri wake,” alisema.
Alisema
kutokana na mgomo uliomalizika wanaimani kwamba kilio chao kimewafikia
wahusika na kwamba kamati hiyo itasimamia kwa weledi ili kuendelea
kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili.
Hali ya Kituo
Meneja
wa kituo hicho, Juma Idd alisema idadi kubwa ya watu waliokuwa ndani ya
kituo hicho kipindi chote cha mgomo iliwapa changamoto kubwa.
“Watu
walikuwa wengi kupita kawaida, kwa sababu wengi ni wageni hawajui kama
hapa kituoni tuna majengo matano ya vyoo ambayo yanajumla ya matundu….
Ilibidi tuwaelekeze watu sehemu hizo,” alisema.
Idd
alisema anamshukuru Mungu kwamba licha ya mgomo huo kuwepo kwa takriban
siku mbili, huduma ya maji ilikuwepo katika kipindi chote na hivyo vyoo
hivyo kufanyiwa usafi kila mara kwani hali ingeweza kuwa mbaya zaidi.
Akizungumzia
juu ya kupanda kwa gharama za vyakula kituoni hapo alisema Halmashauri
haihusiki na jambo hilo kwani huduma hiyo hutolewa na watu binafsi.
“Watu
walikuwa wakilalamika kupanda kwa gharama za chakula, kuna msemo
wanasema kufa kufaana pengine wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao
waliona watumie mwanya huo kujipatia faida na labda kwa sababu bidhaa
zilikuwa hazipelekwi sokoni ikapelekea kupanda kwa gharama za manunuzi,” alisema.
CHAKUA watoa Wito
Katibu
Msaidizi wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) Godwin Ntongeji alitoa
wito kwa wamiliki wa mabasi kutochukua nauli kwa abiria iwapo wanajua
madereva wao watafanya mgomo.
Aliwataka
wamiliki hao kufunga kabisa vituo vyao ili abiria wasikate tiketi
kuliko kuwasababishia usumbufu kama huo walioupata kituoni hapo katika
kipindi hicho cha mgomo.
“Vyakula
vilipanda bei, wengine walikuwa wanakwenda msibani ikashindikana, na
kuna mwanamke mmoja alikuwa mjamzito akapatwa na uchungu ghafla usiku
ilibidi wanawake wenzake wamsaidia walikwenda naye pembeni wakamzingira,
wakamzalisha kisha akakimbizwa hospitalini,” alisema.
Chama cha Madereva wa Maroli
Mwenyekiti
wa Chama cha Madereva wa Maroli (Chamamata), Clement Masanja, alisema
watawashtaki wamiliki wote ambao watawafukuza madereva wao.
Alisema kitendo cha wamiliki kuanza kuwafukuza madereva ni cha uonevu kwani walikuwa wanadai haki zao za msingi.
“Tutafuatilia
kujua kama huyo dereva aliyefukuzwa aliajiriwa kwa mkataba na kama
hakuwa nao sisi kama chama tunao uwezo wa kumshtaki,” alisema Masanja.
No comments:
Post a Comment