WAFANYABIASHARA wadogo na waendesha bodaboda wanaofanya biashara zao
kwenye njia kubwa za kusafirishia umeme wapo hatarini kupungukiwa nguvu
za kiume.
Kutokana na kuwepo wengi kwenye njia hizo kubwa za kusafirishia
umeme, wametahadharishwa kutoendelea kufanya biashara kwenye maeneo
hayo.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mahusiano Msaidizi huduma kwa wateja
wa Tanesco Mwanza, Haji Bwegege wakati akizungumza na waandishi wa
habari baada ya uzinduzi wa maonyesho ya siku ya wafanyakazi uliofanywa
na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kwenye viwanja vya Furahisha,
jijini hapa.
“Tumekuwa tukiielimisha jamii mara kwa mara kutofanya biashara kwenye
njia ya umeme mkubwa unaopita kutokana na madhara wanayoweza kuyapata
na hii ya kupungukiwa nguvu za kiume ni moja ya madhara ambayo yanaweza
kuwapata hivyo wachukue tahadhari mapema,” alisema.
Aliyataja madhara mengine kuwa pamoja na mwili kupoteza nguvu
kutokana na mionzi hivyo wananchi kutakiwa kuishi umbali wa mita 30 kila
upande pamoja na mjamzito kuharibu mimba.
Akizungumzia suala la ‘Vishoka’, Bwegege aliwataka wananchi
wasikubali kuuziwa fomu majumbani kwani fomu za kuomba kuunganishiwa
umeme hutolewa ofisini tu ama pale maofisa wao wanapotembelea vijijini
wakiwa na vitambulisho na kutoa risiti.
“Mnatambua kuwa miradi ya umeme vijijini inaendelea ya Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) na Electricity five (F5) hivyo vishoka kutumia
nafasi hiyo kuwarubuni wananchi ambapo wamekuwa wakifika vijijini na
kuwauzia fomu kati ya Sh 60,000 na 100,000 wakati bei halisi ya fomu ni
Sh 5,900 tu,”alisema.
Alisema vishoka hao wamekuwa wakijitokeza katika maeneo ya vijijini
ambapo miradi hiyo imekuwa ikiendelea na kwamba kama Tanesco wamekuwa
wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara na
kuwataka wananchi wajiandikishe kwenye ofisi za serikali za vijiji.
Bwegege alisema chini ya miradi ya wakala wa umeme vijijini, wananchi
wanaozungukwa na mradi hutozwa Sh 27,000 kama gharama ya kuungiwa
umeme.
Alisema wameshiriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa jamii
juu ya shughuli zao na kwamba huduma zote zinazotolewa ofisini
zinatolewa uwanjani hapo.
No comments:
Post a Comment