Mwanachama atakayetaka kuwania urais kwa tiketi ya Chadema
atatakiwa kulipia Sh1,000,000 za fomu, ambazo atarejeshewa iwapo
hatapitishwa kuwa mgombea pekee wa vyama vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), chama hicho cha upinzani kilisema jana.
Sera hiyo ya kurejesha fedha pia itahusu watu
wengine watakaotaka kuwania ubunge na udiwani baada ya Chadema na vyama
vingine vitatu vya upinzani, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kukubaliana
kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Chama hicho kikuu cha upinzani pia kimeweka
utaratibu wa wagombea ubunge kujitathmini iwapo kutakuwa na mgombea
zaidi ya mmoja kwa kuwapa nafasi ya kujipigia kura kabla ya vikao vya
uamuzi kutumia kura hiyo kama maoni yatakayosaidia kumteua mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu
alisema kwamba wagombea wa urais watachukua fomu makao makuu kuanzia
Julai 20 na kuzirudisha Julai 25.
Pia, katika uchaguzi wa rais mwaka 2010, mgombea
wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura
2,271,941, ambazo ni sawa na asilimia 26.34 akiwa nyuma ya Rais Jakaya
Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Hadi sasa Dk Slaa hajatangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Chadema na hakuna mwanachama aliyeonyesha nia hiyo.
Kuhusu fomu za nafasi ya ubunge wa jimbo na
ubunge wa viti maalumu, Mwalimu alisema zitatolewa kwa gharama ya
Sh250,000, huku fomu za udiwani wa kata na wa viti maalumu zitagharimu
kiasi cha Sh50,000 na fomu hizo watazichukulia kwa makatibu wa majimbo
na makao makuu ya chama hicho.
“Huu ni uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema,” alisema Mwalimu bila ya kufafanua vigezo walivyotumia kuweka viwango hivyo.
Hadi sasa Chadema inaongoza upinzani kwa kuwa na wabunge 45, kati yao 23 ni wa viti maalumu.
Mwalimu alisema kuwa wagombea wa nafasi za ubunge
wataanza kuchukua fomu kuanzia Mei 18 na kuzirudisha Juni 25, wakati
kwenye sehemu ambazo zina wabunge, kazi hiyo itaanza Julai 6 na
kumalizika Julai 10, kipindi ambacho Bunge la 10 litakuwa limevunjwa.
Pia, alisema kwamba wagombea udiwani wataanza
kuchukua fomu kuanzia Mei 18 na kuzirejesha Juni 25 na watazipata kwenye
ofisi za makatibu wao wa kata za jimbo pamoja na wilaya husika.
Mwalimu alitoa wito kwa wananchi ambao ni
wanachama wa Chadema wenye sifa wajitokeze kuwania nafasi hizo na kwamba
vyombo husika vitazingatia matakwa ya katiba ya chama hicho kwa kuwa
lengo ni kupata wagombea waadilifu wenye uwezo wa kuwatumikia watu na
wanaokubalika kwa wapigakura.
Kuhusu kurejeshewa fedha za kuchukulia fomu, Mwalimu alisema
uamuzi huo utahusu wanachama watakaokuwa wamepitishwa na Chadema, lakini
wakakosa kuteuliwa na Ukawa.
“Chadema itabeba jukumu la kumrejeshea pesa zake
alizochukulia fomu ikiwa kwa bahati mbaya Ukawa itampitisha mwingine,
lakini ikiwa yeye mwenyewe atasema zibaki kwa ajili ya maendeleo ya
chama basi zitatumika kwenye maendeleo,” alisema Mwalimu ambaye
kitaaluma ni mwandishi wa habari.
“Kila mgombea atapewa nafasi ya kujieleza mbele ya
wapigakura, atajieleza kwa dakika tano na ataulizwa maswali yasiyozidi
matatu kutoka kwa washiriki na kura zitakazopigwa baada ya wagombea wote
kujieleza mbele ya mkutano maalumu,” alisema. Aliongeza kuwa kila
mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kuhesabu kura zake.
Akizungumzia utaratibu wa kuwapata wagombea,
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri Kuu ya Chadema, John Mrema alisema
wagombea wote watapewa fursa ndani ya mkutano maalumu kujipigia kura.
“Kila mgombea atatakiwa apige kura mara tatu iwapo
kutakuwa na mgombea zaidi ya mmoja, moja itakuwa yake binafsi na kura
nyingine atatakiwa kumpigia mgombea mwingine anayeona anafaa kati ya
waliojitokeza,” alisema Mrema.
No comments:
Post a Comment