Kikwete Amtega Nkurunziza.....Wabunge Wa Burundi Wahofia Usalama Wao, Wazamia Arusha - LEKULE

Breaking

28 May 2015

Kikwete Amtega Nkurunziza.....Wabunge Wa Burundi Wahofia Usalama Wao, Wazamia Arusha


RAIS wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewekwa mtegoni baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Jakaya Kikwete, kuitisha mkutano wa wakuu wa nchi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Makao Makuu ya EAC jijini Arusha, kikao hicho cha dharula kinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Jumapili hii.

Huu unachokuliwa kama mtego kwa Nkurunziza ambaye wakati wa kikao kingine kama hicho kilichofanyika Mei 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam, wanajeshi nchini humo, chini ya shushushu namba moja wa zamani wa nchi hiyo, Meja Jenerali Godfroid Niyombare, walifanya jaribio la kupindua serikali yake.

Pamoja na Rais Nkurunziza na Kikwete, kikao cha wakuu wa nchi za EAC hujumuisha pia marais Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda) na Uhuru Kenyatta wa Kenya, ingawa pia viongozi wa nchi nyingine wanaweza kualikwa hasa katika suala kama hili la mzozo nchini Burundi.

Nkurunziza alilazimika kukaa mafichoni jijini Dar es Salaam hadi baada ya wanajeshi wanaomtii kujibu mashambulizi na kumaliza mapinduzi hayo.

Tangu wakati huo, kumekuwa na maandamano na vurugu nchini Burundi kupinga mpango wa Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais, huku vifo kadhaa vikiripotiwa.

Na sasa, wakuu wa nchi hizo wanatazamiwa kukutana tena Jumapili hii kwa mzunguko wa pili wa mazungumzo ya kutafuta utatuzi wa mzozo huo.

Wito wa Kikwete kwa Nkurunziza unachukuliwa kama mtego na kuna kila dalili kuwa huenda asihudhurie ingawa kukosekana kwake kutapunguza ushawishi ambao angeweza kuufanya kwa viongozi wenzake ambao miongoni mwao, kama Uhuru wa Kenya, wanakosoa uamuzi wake wa kugombea muhula wa tatu.

Taarifa katika mitandao kadhaa zilimnukuu msemaji wake, Gervais Abayeho, akisema nchi hiyo itatuma wawakilishi; “kwa sasa ni mapema kufahamu ni akina nani watakaoiwakilisha Burundi.”

Mbali na Rais Uhuru Kenyatta, viongozi kadhaa wa Afrika walimshauri Nkurunziza kuheshimu matakwa ya raia wake huku Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini akisema: “Nkurunziza asipoachana na mpango wake huo, atalilirudisha taifa lake kwenye vita.”

Wabunge wa EALA wazamia Arusha
Wakati Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ikijiandaa kutembelea Burundi kujionea madhara yaliyosababishwa na mzozo unaoendelea, kuna taarifa kuwa wabunge kadhaa wa Bunge hilo kutoka Burundi bado wapo jijini Arusha.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa wabunge watatu au wanne kati ya tisa waliokuwa wakishiriki kikao cha EALA wanaendelea kuishi nchini.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wabunge hao alisema wameshindwa kurejea nyumbani kutokana na hali mbaya ya usalama iliyopo huko.

“Tumekuwa tukiwasiliana na wenzetu Burundi na wametuambia si salama sana kwa sasa kurejea huko, ndio maana bado tupo hapa,” alisema Mbunge huyo.

Wiki iliyopita EALA ilimaliza kikao cha wiki mbili jijini Arusha na wabunge kutoka mataifa mengine waliondoka Jumamosi.

Mbunge huyo hakuwa tayari kueleza ni nani anawalipia gharama za hotelini kwa sasa na kwa muda gani wataishi nchini.

Wabunge tisa wanaoiwakilisha Burundi EALA ni Emerence Bucumi, Hafsa Mossi, Isabelle Ndahayo, Leonce Ndarubagiye, Martin Nduwimana, Emmanuel Nengo, Jeremie Ngendakumana, Frederic Ngenzebuhoro na Yves Nsabimana.

No comments: