Nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa jana zilichunguza mgogoro wa Burundi katika kikao
chao cha faragha. Awali mwakilishi wa Russia katika Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa alisusia hatua yoyote ya kuchukuliwa msimamo wa upande
mmoja dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi. Mwakilishi wa Russia
anaamini kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halipasi kuingilia
masuala yanayohusiana na katiba za nchi au kukiuka mamlaka ya kujitawala
nchi mbalimbali. Kikao hicho cha Baraza la Usalama kuhusiana na mgogoro
wa Burundi kimefanyika kufuatia ombi lililotolewa na Francois Delattre,
mwakilishi wa Ufaransa katika baraza hilo.
Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia
Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa raia karibu elfu
50 wa Burundi wameikimbia nchi hiyo na kuelekea katika nchi jirani.
Takwimu za UNHCR zinaonyesha kuwa raia wa Burundi wanaokaribia elfu 25
wamewasili Rwanda, 7700 wamekimbilia Tanzania na wengine 8000 wameelekea
katika mkoa wa Kivu ya Kusini huko mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Wakimbizi wengi wa Burundi wamekiri kuwa
wameikimbia nchi yao kwa kuhofia kukandamizwa na na mashambulizi ya
wanamgambo na wafuasi wa chama tawala cha CNDD-FDD. Vijana hao wafuasi
wa chama tawala wanaojulikana kwa jina la "Imbonerakure" wanatuhumiwa
kuchochea ghasia na kuuwa raia wa Burundi.
Katika mazingira hayo, wakuu wa vyama
vya upinzani na wawakilishi wa serikali ya Burundi pia jana walikutana
kwa mara nyingine na kufanya mazungumzo. Mazungumzo hayo yamefanyika
lengo likiwa ni kufikia mwafaka ili kusitisha maandamano ya wananchi
dhidi ya serikali ambayo yalianza huko Bujumbura mji mkuu wa Burundi
tangu tarehe 25 mwezi Aprili. Uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza ya
kutangaza nia yake ya kuwa mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa
Rais uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi Juni mwaka huu umekabiliwa na
upinzani mkali kutoka kwa vyama vya upinzani, makundi ya kiraia na hata
watu wa kabila la Wahutu ndani ya chama tawala cha CNDD-FDD.
Watu wasiopungua 18 wakiwemo polisi
kadhaa, wamepoteza maisha katika ghasia zilizoibuka kati ya vikosi vya
polisi na waandamanaji wanaopinga hatua ya Rais Nkurunziza ya kugombea
kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu. Vyama vya upinzani Burundi
vimewatolea wito wafuasi wao kufanya maandamano ya amani dhidi ya kile
walichokiita kuwa ni mapinduzi, tangu Rais Nkurunziza atangaze uamuzi
wake huo. Vikosi vya usalama vya Burundi pia mbali na kuyakandamiza
maandamano ya wananchi, vimemtia mbaroni Pierre Mbonimpa mmoja wa
viongozi wa jumuiya za kiraia nchini humo.
Jenerali Gabriel Nzigama Waziri wa
Usalama wa Ndani wa Burundi amewatuhumu waandamanaji kuwa wanafanya
vitendo vya kigaidi. Hata hivyo Jenerali Gaciyabwenge ambaye ni Waziri
wa Ulinzi wa Burundi ametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo halipendelei
upande wowote katika mivutano inayoendelea kati ya waandamanaji na
vikosi vya usalama. Baada ya Waziri wa Ulinzi wa Burundi kutamka hayo,
Mkuu wa Majeshi ya Burundi pia aliwataka wanajeshi nchini kuwa watiifu
kwa serikali.
Mivutano ya kisiasa nchini Burundi
imeshtadi tangu tarehe 5 mwezi huu baada ya majaji sita wa Mahakama ya
Katiba kumuidhinisha Rais Nkurunziza kuwa mgombea katika uchaguzi ujao.
Jaji wa saba wa mahakama hiyo ambaye hakuwa tayari kumuidhinisha
Nkurunziza, amekabiliwa na mashinikizo ya kisiasa na kutishiwa kuuawa
na hatimaye ameamua kutoroka nchini.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamisheni
ya Umoja wa Afrika Bi Nkosazana Dlamini Zuma juzi alisisitiza kuwa hali
ya usalama nchini Burundi haifai kwa ajili ya uchaguzi wa wazim huru na
wa kiadilifu. Viongozi wa nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) wamemtaka Rais wa Burundi ajiondoe katika kinyang’anyiro
cha urais.
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
wanatazamiwa kukutana mjini Arusha, Tanzania tarehe 13 mwezi huu
kujadili mgogoro na machafuko ya Burundi na taathira zake katika nchi
nyingine za eneo hilo.
No comments:
Post a Comment