JK awasafisha mawaziri waliotimuliwa na Bunge - LEKULE

Breaking

9 May 2015

JK awasafisha mawaziri waliotimuliwa na Bunge


Baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye Ikulu imewasafisha mawaziri wanne walioshinikizwa na Bunge kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili, Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini waliohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Waliotangazwa kuwa safi ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wawili hao wanatajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM ingawa hawajatangaza nia.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo.

Hali kadhalika, Profesa Sopster Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ametangazwa kuwa safi pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi, ambao walihusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Uamuzi wa Ikulu kuwaondolea doa hilo mawaziri hao wanne umetokana na ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo iliyolenga kuondoa ujangili kwenye hifadhi za Taifa, lakini ikaishia kuua wananchi, kutesa na kupora mali zao.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliwaambia wanahabari kuwa tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete ilijiridhisha kuwa mawaziri hao  waliwajibika kisiasa na hawakuhusika moja kwa moja na vitendo hivyo na hakuna hatua inayostahili kuchukuliwa dhidi yao.

Rais Kikwete aliunda tume hiyo Mei mosi mwaka jana kuchunguza malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Operesheni hiyo ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utali kwa lengo  la kupambana na ujangili ambao ulikithiri hadi  taasisi za kimataifa kuingilia kati. Hata hivyo ilisitishwa Novemba Mosi, 2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko yaliyojitokeza.

Tume hiyo ilikuwa na makamishna watatu, ikiwa chini ya uenyekiti wa Balozi Hamisi Msumi, Jaji Stephen Erenst, Jaji Vicent Kitubio na Frederick  Lema ambaye alikuwa katibu.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Balozi Sefue alisema licha ya  mawaziri hao kuonekana wasafi, bado tume ilibaini ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu  katika utekelezaji wa operesheni hiyo.

Madhara ya operesheni

 Balozi Sefue alisema Tume hiyo ilichunguza matukio 15 ya vifo na kuridhika kuwa vifo tisa  kati ya hivyo, vilisababishwa na mateso kutoka kwa watendaji wakati wa operesheni. 

“Watendaji kwenye operesheni walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji. Kabla ya vifo, watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu na wa kimazingira unaohusisha vifo vyao,” alisema Balozi Sefue.
Kadhalika  ripoti ya Tume hiyo iliridhika na ushahidi kuwa wananchi waliteswa na kudhurika kimwili wakati walipolazimishwa kuonyesha silaha zilipofichwa, au kulazimishwa kukiri kuhusika na ujangili au kushinikizwa wawataje washirika wao wa mtandao wa ujangili.
Sefue alisema katika malalamiko hayo yaliyotoka katika wilaya 22 za mikoa mbalimbali, wananchi waliwasilisha uthibitisho wa kuteswa na walionyesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na hati za kuripoti vitendo hivyo polisi (PF 3) walizopewa baada ya kuumia.
Tume hiyo pia ilionyesha kuwa kulikuwa na tuhuma za wizi, upotevu na uporaji wa mali na walalamikaji walidai kuibiwa au kupoteza fedha na mali zao wakati wa kupekuliwa au kukamatwa na askari wa Operesheni.
“Tume ilichunguza jumla ya matukio 23 ya aina hiyo na kubaini kuwa malalamiko mengi yalitokana na askari wa operesheni kutofuata sheria, kanuni na taratibu za ukamataji,” alisema Balozi Sefue.

Uchomwaji wa nyumba na ubakaji
 Akisoma ripoti hiyo, Balozi Sefue alisema tume ilibaini  kuwa baadhi ya askari wa Operesheni walichoma nyumba moto kwa madai kuwa zilijengwa kwenye hifadhi.
Malalamiko hayo yalitoka wilaya za Mlele na Mpanda mkoani Katavi, Momba (Mbeya), Nkasi, Sumbawanga (Rukwa) na Wilaya ya Simanjiro mkoani Arusha.
“Katika uchunguzi wa matukio hayo, tume ilibaini wanakijiji hawakupewa taarifa za kutosha kuhusu mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao na katika harakati hizo wanavijiji walipoteza mali na vyakula vyao,” alisema.
Hata hivyo, kwa upande wa malalamiko ya ubakaji ambayo Tume iliyachunguza, waliodai kubakwa hawakujitokeza kutoa ushahidi na badala yake alijitokeza mlalamikaji mmoja ambaye maelezo yake hayakujitosheleza.

Askari walipora bunduki
Akichambua zaidi taarifa ya Tume hiyo, Balozi Sefue alisema ushahidi unaonyesha kuwa askari wa Operesheni walikamata au kuchukua bunduki, risasi pamoja na vitabu vyake  hata kama vilikuwa vikimilikiwa kihalali.

Alisema katika baadhi ya maeneo, askari hao waliua ng’ombe kwa kuwapiga risasi na wengine waliuzwa kwa mnada bila kuzingatia taratibu za kisheria.

Kuhusu Profesa Muhongo na Maswi, Balozi Sefue alisema waziri huyo wa zamani wa nishati na madini alionekana hana hatia na ndio maana hakupelekwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo pia ilimchunguza Maswi na kumuona kuwa hakuhusika katika uchotwaji huo wa fedha wala kupata mgawo.

Lakini mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliibeza ripoti hiyo akidai kuwa ofisi hiyo kuu ya nchi ni sehemu ya wahusika wa tuhuma hizo.

“Kuna ushahidi usio na mashaka kuwa Ikulu inahusika na sakata la escrow kutokana kuwapo barua kutoka kwa Maswi kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu uhamishaji haramu wa fedha za umma. Kitendo cha Balozi Sefue kumsafisha Maswi hakishangazi kwa sababu yeye pia ni mhusika,” alisema Kafulila,

Alifafanua kuwa Sefue ndiye katibu wa Baraza la Mawaziri na hakuna kumbukumbu yoyote inayoonyesha kuwa aliwahi kuitaarifu baraza hilo uwepo wa kashfa ya escrow.

Balozi Sefue alizungumzia suala la Profesa Muhongo baada ya kuulizwa swali kwa kuwa suala hilo halikuwamo kwenye taarifa yake.

Kuhusu Maswi, alisema matokeo ya Uchunguzi yanaonyesha hakuwa na maslahi binafsi katika uamuzi wake wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutolewa.

Kadhalika Sekretarieti  haikubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma, bali  ilibaini kuwa alichokifaya kilizingatia matakwa ya Sheria na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ridhaa ya Tanesco.

“Kwa  maana hiyo, Sekretariati ya Maadili haikuona msingi wowote wa kuendelea na shauri la Maswi na wamelihitimisha,” alisema Sefue.

Operesheni ilikuwa na mafanikio

Hata hivyo, Tume inabainisha kuwa pamoja na makandokando hayo lakini katika kipindi cha mwezi mmoja tangu  ilipoanzishwa Oktoba 4, 2013,  watuhumiwa zaidi ya 1,030 wenye makosa ya ujangili na uvunaji haramu wa misitu walikamatwa.

Balozi Sefue alieleza kuwa wakati wa Operesheni hiyo, meno 211 ya tembo yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama 36, ngozi za wanyama 21, pembe za swala 46, mitego 134 ya wanyama, ng’ombe 7,621 waliokuwa wakichungwa ndani ya hifadhi, walikamatwa.

Pia, alitaja mafanikio mengine ya Operesheni hiyo kuwa ni kukamatwa kwa silaha zikiwemo bunduki 18 za kijeshi, bunduki 1,579 za kiraia na risasi 1,964.

Uamuzi wa Serikali

Sefue alisema baada ya kupitia taarifa ya Tume, serikali itachukua hatua za kimashtaka kwa shauri la mauaji ambalo upelelezi wake umekamilika.

Pia hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa opereshani.

Pia, Takukuru inaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa na udanganyifu.

“Wale waliopoteza ndugu au kupata madhara makubwa ya mwili, serikali lazima itawapoza,” alisema Balozi Sefue.

Katika mkutano wake wa 16 na 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilijadili taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na taarifa ya Ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Bunge lilipitisha maazimio  na kumtaja Maswi kuhusika kijinai au kimaadili katika miamala  ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Baadaye Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akihutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam alisema amezielekeza mamlaka kuchunguza tuhuma dhidi ya Maswi  na kufafanua kuwa iwapo itabainika basi hatua za kinidhami zitachukuliwa.

Wakati huohuo, Rais amesaini sheria kadhaa ikiwemo Sheria ya Ajira kwa Wageni, Sheria ya Marekebisho ya  Sheria ya Ardhi na Nyumba, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Baraza la Vijana, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki.

No comments: