Ni dhahiri sasa kuwa hatua ya vikao vya juu vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa wamefungiwa kwa kuanza kampeni mapema na kutangaza tarehe za kuanza kuchukua fomu, vimechochea harakati za kusaka urais na kuongeza urefu wa foleni ya wanaotaka kuelekea Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya siku nne baada ya uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada wake, kuanza kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa wanatangaza nia hiyo wiki ijayo.(P.T)
Wakati Makongoro akisema sasa anajisikia kuomba kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni 3, Profesa Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku Profesa Mwandosya akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa mada hao ambao kwa muda mrefu hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha ya makada waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita 'safari ya matumaini' Jumamosi mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa atafanya hivyo hivi karibuni huko Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili aweze kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali.
Katika mlolongo huo wapo makada waliokuwa wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana ni hiyo ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi, mbunge huyo wa Afrika Mashariki alisema: "Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza Watanzania katika ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa kufanya hivyo vinaniruhusu."
Makongoro alisema hayo wakati akitoa shukrani kwa viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka kazi alizofanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na machifu walioshiriki hafla hiyo, walimtaka Makongoro 'kuvunja tetesi' zinazosambazwa kupitia vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na kumtaka atamke wazi juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa Busokelo, Prince Mwaihojo alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo mazito akiwa mkoani hapo.
No comments:
Post a Comment