Dar es Salaam.
Mawaziri wakuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba wameonya kuwa hali ya mgawanyiko, ubaguzi wa kidini, ukabila na ujimbo miongoni mwa wananchi inatishia umoja na utulivu wa nchi iwapo hatua hazitachukuliwa.
Mawaziri wakuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba wameonya kuwa hali ya mgawanyiko, ubaguzi wa kidini, ukabila na ujimbo miongoni mwa wananchi inatishia umoja na utulivu wa nchi iwapo hatua hazitachukuliwa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti katika mkutano wa siku mbili wa mashauriano kuhusu
amani na umoja nchini ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF)
jana, viongozi hao walisema misingi ya amani na utulivu iliyojengwa
nchini inastahili kulindwa.
Katika siku za karibuni,
viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu walitofautiana katika ahadi ya
Serikali kuingiza Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba, suala la Muungano
likisababisha mjadala mkali bungeni, huku kukiwa na mapigano ya mara kwa
mara ya wafugaji na wakulima.
Dk Salim, ambaye ni
mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa MNF, alisema Watanzania wengi wana
wasiwasi kuwa amani, umoja na utulivu uliopo hivi sasa nchini unaweza
kutoweka iwapo hawatailinda misingi hiyo.
Akifungua
mkutano huo uliowakutanisha viongozi wakuu wa Serikali waliopo na
wastaafu, viongozi wa dini, wazee na viongozi wa vyama vya siasa, Dk
Salim alisema: “Katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano Watanzania
tuache ubaguzi na kubaguana kwa hisia za kiitikadi, dini, ukabila,
mahali mtu anatoka, kazi anayofanya au uwezo wake kiuchumi.
“Na
kamwe tusifikiri kuwa amani na umoja ni vitu ambavyo vipo tu… ukiona
kuna amani na umoja ujue kuwa zilifanywa jitihada, tena jitihada za
kweli kweli.”
Alisema kwa kuwa lengo la vyama vya siasa
ni kutawala, haiwezekani kuwa na utawala bora bila kuwa na amani, umoja
na mshikamano katika jamii.
“Tanzania ikipata
matatizo hakuna atakayepona. Biashara haiwezekani katika mazingira
ambayo nchi haina amani na utulivu; kilimo na ufugaji haviwezekani penye
fujo,” alisema Dk Salim ambaye pia amewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa
Nchi Huru za Afrika (OAU).
Jaji Warioba
Akizungumza
katika mkutano huo, Jaji Warioba alisema hivi sasa jamii imetawaliwa na
udini, ukabila na ukanda na kwamba hata viongozi hawataki kuitwa
‘ndugu’ kama ilivyokuwa enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Maneno
kama ndugu yalikuwa yanaleta usawa, leo ukimwita kiongozi ndugu anaona
umemdharau,” alisema Jaji Warioba na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya
kwanza ilitaifisha shule za dini ili kuleta usawa na umoja lakini hivi
sasa hali hiyo imeanza kuondoka.
“Siku hizi ukiniuliza
mimi nitakwambia kabila langu fulani, dini yangu ni fulani, natokea
ukanda fulani, elimu yangu ni fulani, tumeanza kubaguana,” alisema.
Mkurugenzi
mtendaji wa MNF, Joseph Butiku alisema mkutano huo haukusudii kumtafuta
mchawi anayetishia kutoweka kwa amani, bali kuzungumza kwa uwazi bila
kunyoosheana vidole.
Alisema mazungumzo yatafanyika
katika makundi matatu tofauti na wote watajadili viashiria vya kutoweka
kwa amani nchini na namna ya kuepukana na hali hiyo.
“Tutajaribu kujibu swali ‘tufanye nini?’. Kikao hakitakuwa na faida kama hatutaweza kujibu swali hilo,” alisema Butiku.
Akitoa
salamu kwa niaba ya viongozi wa siasa, mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alisema hakuna namna Taifa linaweza kuwa na amani kama
hakuna haki.
“Ninaamini kikao kitakapomalizika kitatoa mwongozo kwa Taifa kuhakikisha haki inatendeka,” alisema Profesa Lipumba.
Hata
hivyo, Profesa Lipumba alisema amesikitika kwa viongozi wa CCM waliopo
madarakani kutokuhudhuria katika mkutano huo unaojadili amani.
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema migogoro iliyopo nchini na
mpasuko wa kidini umechangia kuondoka kwa amani na hivi sasa wananchi
wengi hawaaminiani.
“Viongozi wa dini hawaaminiani,
wazee hawaaminiani, serikalini nao hawaaminiani, wachochezi wanaoondoa
amani kwa kiasi kikubwa ni viongozi,” alisema Mbatia.
Mwenyekiti
wa Chama cha Saidia Wazee Tanzania (Sawata), Brigedia Jenerali Francis
Mbena alisema ili amani iendelee kuwapo nchini, wazee lazima watumiwe
kutoa ushauri.
No comments:
Post a Comment