Dodoma/Dar. Bunge la Bajeti ya Serikali ya 2015/16 linaanza
leo mjini Dodoma kwa mwendo wa mchakamchaka kutokana na kuongezwa saa
mbili kila siku ili limalizike Juni 27.
Saa za mjadala
katika vikao zimeongezwa ili kuziba pengo la siku 12 zinazopungua na
kutoa fursa kwa wabunge kuchangia bajeti za wizara na Bajeti Kuu ya
Serikali ndani ya siku 44 ikilinganishwa na siku 56 zilizotumika
kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15 na miaka ya nyuma.
Kutokana
na hali hiyo, wachambuzi wa bajeti, wachumi na wanasiasa wamesema
hawatarajii kuona jipya isipokuwa mipasho inayolenga Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh22.4
trilioni katika mwaka wa fedha 2015/16 ikiwa ni nyongeza ya Sh2.6
trilioni ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa Sh19.8
trilioni.
Kwa miaka iliyopita, baadhi ya wizara zenye
majukumu mengi zilikuwa zinatengewa siku mbili au tatu, lakini safari
hii hali itakuwa tofauti kwa kuwa zitajadiliwa kwa siku moja tu au mbili
kulingana na mjadala utakavyokuwa na mapumziko yatakuwa Jumapili pekee.
Mkurugenzi
wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey
Mwakasyuka alisema badala ya Bunge kuanza saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00
mchana na baadaye saa 11 jioni hadi saa 1.45 usiku; sasa litaanza 3.00
asubuhi hadi saa 8.00 mchana na kuendelea saa 10.00 jioni hadi saa 2.00
usiku.
“Ili kuendana na muda, tumeongeza saa kadhaa ili
kumaliza shughuli zote zilizopangwa. Siku za Jumamosi zitahesabika kama
siku za kazi kama kawaida.” alisema.
Alisema Bunge
hilo litamalizika Juni 27 lakini akaongeza: “Tumeacha siku tatu za
dharura, kuanzia Juni 28 hadi 30 ili kama kuna jambo lolote la muhimu
litajitokeza Bunge linaweza kuendelea kwa muda huo wa siku tatu.”
Alisema
kutokana na mabadiliko ya uwasilishaji, ni lazima bajeti iwe imesomwa
kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka unaofuata Julai Mosi.
“Inawezekana
tukapata kiongozi wa kulihutubia Bunge au katika upitishaji wa bajeti
za wizara akidi isitimie na kulazimika shughuli husika kuendelea siku
inayofuata. Zamani Bunge la Bajeti lilikuwa likianza Juni hadi Agosti,
lakini kwa mabadiliko haya sasa lazima limalizike Juni,” alisema.
Alisema
bajeti zote za wizara hadi kufikia Juni 10 zitakuwa zimeshasomwa, Juni
11 itasomwa Bajeti Kuu ya Serikali na kuanza kujadiliwa.
Alisema ratiba hiyo pia inaweza kuvurugika utakapoanza mfungo wa Ramadhani.
Alisema kuchelewa kuanza kwa Bunge kumetokana na kuahirishwa kwa tarehe ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
“Kama
mtakumbuka Katiba Inayopendekezwa ilikuwa ipigiwe kura Aprili 30, sasa
baada ya kutangazwa kuwa imeahirishwa, tuliamua kupanga upya ratiba,”
alisema.
Alisema Bunge hilo litavunjwa kwa tangazo la
Serikali linalotolewa na Rais na si Mkuu huyo wa Nchi kulihutubia Bunge
na kulivunja: “Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atalihutubia Bunge Juni 27.”
Maoni ya wasomi
Profesa
Prosper Ngowi kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema
mbali na Bunge hilo kutekwa na mijadala ya kuelekea uchaguzi ujao, mambo
mengine yanayotarajiwa ni wabunge wengi kuonyesha mbwembwe za kuhoji
mambo yanayohusu masilahi ya wananchi katika majimbo yao.
Alisema
wabunge watakuwa na hoja za kuibana Serikali juu ya miradi mingi
iliyokwama katika bajeti zilizopita kutokana na kiwango kidogo cha fedha
kilichowasilishwa.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Profesa
Humphrey Moshi kutoka Idara ya uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) akisema wabunge watahoji utekelezaji wa bajeti iliyopita kwa
kuangalia uhalisia wake na mipango ya bajeti itakayojadiliwa kwa Bunge.
“Kila
mbunge anatamani kuona mradi wa maendeleo ukikamilika katika jimbo
lake, lakini ukiangalia fedha ambazo zimekuwa zikitengwa ni kidogo na za
utegemezi, kwa hivyo ningeshauri kwa sasa wangejadili na kushughulikia
viporo vya miradi, badala ya kuanzisha vingine wakati kuna madeni ya
makandarasi,” alisema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa
Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi Tanzania (CEOs), Ali Mufuruki alisema
hatarajii kuona jambo lolote jipya zaidi ya mijadala ya kuelekea
Uchaguzi Mkuu.
“Ninachotegemea kwa sasa ni kuona sehemu kubwa ya mapato yakitumika kwa shughuli za kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.
Wabunge wanena
Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema bajeti hiyo
haina matumaini kwani miradi ya maendeleo katika bajeti inayomalizika
Juni 30 haikutekelezeka kwa asilimia 80.
“Kukwama kwa
msaada wa kibajeti zaidi ya Dola 500 milioni kutoka kwa wahisani,
kukwama kwa mkopo wa kibiashara ambao siyo kawaida kabisa ambapo
Serikali ilitarajia kukopa Dola 800 milioni na kuambulia 300 milioni ni
ushahidi tosha wa namna Serikali inavyopumulia mashine,” alisema.
Mbunge
wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla alisema muda wa kuijadili bajeti
ni mfupi hali ambayo hujitokeza kila mwaka wa uchaguzi lakini haiwezi
kuwanyima wananchi fursa ya kuijua bajeti ya nchi yao.
Mbunge
wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alisema bajeti hiyo haina
jipya, huku akitolea mfano mpango wa Serikali wa kuboresha reli kwa
mwaka mmoja wakati ilishindwa kufanya hivyo kwa miaka 50.
Mbunge
wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alisema tatizo la bajeti hii ni
kupunguzwa kwa asilimia 50 fedha za maendeleo... “Unapopunguza fedha za
maendeleo wakati tunaambiwa bwawa la umeme la Mtera maji yamepungua hapo
si tutegemee kurudi kule kwa Aggreko na Symbion kuuziwa umeme wa
ghali.”
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba alisema fedha za maendeleo ambazo zimepungua zitapatikana kabla
ya Juni 30, mwaka huu... “Niwathibitishie wananchi kuwa fedha hizi
zitapatikana bila matatizo yoyote.”
No comments:
Post a Comment