BILIONI 600 ZIMEPIGWA, AFU KIMYA! - LEKULE

Breaking

22 May 2015

BILIONI 600 ZIMEPIGWA, AFU KIMYA!


TUNAAMBIWA wakati tukipata uhuru mwaka 1961, nchi yetu ilikuwa na uchumi sawa na nchi kama Singapore, Malaysia na nyingine nyingi zilizokuwa dunia ya tatu. Leo tunapojifananisha na nchi hizo za Asia, tunaonekana vichekesho.
Lakini si nchi hizo mbili tu, bali kuna mataifa mengi yamefanya vizuri kiuchumi kuliko sisi, hata kwa zile za Afrika, bara ambalo historia inatuambia watawala wake wametawaliwa na tamaa, ubinafsi, chuki na wivu dhidi ya wanaowaongoza.
Ndiyo maana tulipata vizazi vya watu wa aina Mabotu Sese seko, Idd Amin, Hosni Mubarak, Kamuzu Banda, Charles Taylor na wenzao, ambao waliamini wao ni bora kuliko wengine wote, kiasi cha kujiona kama miungu watu wanaostahili kukaa kileleni milele.
Kinachouma ni kwamba katika bara hili hili, walikuwepo watu walioonekana kuwa watawala bora, wanaoendelea kutajwa na historia kama akina Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Nelson Mandela, Patrice Lumumba, Gamel Abdul Nasser, Jerry Ralwings, Joachim Chissano na wengine wa aina yao.
Wanaotajwa kwa wema, kila mmoja alifanya kitu kwa taifa lake na kwetu sisi, tunapomzungumzia Mwalimu Nyerere kila mmoja anajua nini aliifanyia nchi yake, licha ya wakosoaji wachache kumpinga. Ni katika utawala wa Nyerere pekee ambako Watanzania walipata elimu bora bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.
Ni enzi hizo pekee ambapo nchi ilikuwa na viwanda vingi vilivyomilikiwa na serikali, thamani ya shilingi ilikuwa juu na hali ya maisha iliridhisha, licha ya ukweli kwamba mambo yote hayo, yalitegemea zaidi vyanzo vya mapato vilivyotokana na kilimo.
Leo, viwanda vyote vikiwa vimeuzwa, uchumi wa nchi ukiwa mikononi mwa wageni, miundombinu ya reli ikiwa imeharibiwa makusudi ili kupisha malori ya vigogo kufanya kazi ya usafirishaji, mashirika ya umma yakiwa yamepotezwa ili kuotesha kampuni za viongozi, watawala wameruhusu ukwapuaji mkubwa wa fedha za umma bila kuonesha hata tone la shtuko!
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotolewa mwanzoni mwa wiki hii mjini Dodoma, imeonesha kuwa vigogo wa serikali, kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2014, walijichotea kiasi cha shilingi bilioni 600 kupitia ‘dili’ mbalimbali, kama mishahara hewa, misamaha ya kodi, ununuzi wa kutofuata kanuni, ukwapuaji wa fedha za maafa na udanganyifu mwingine uliofanywa na mamlaka.
Hizi ni fedha nyingi, mara mbili ya zile zilizowaondoa ofisini mawaziri wawili, mwanasheria mkuu wa serikali, katibu mkuu mmoja na viongozi wawili wa kamati za bunge kuvuliwa nyadhifa zao katika kashfa ya Escrow.
Hapa serikali imekaa kimya, kimya kabisa kama haijui lolote, ingawa ripoti imeonesha wapi waliiba nini. Na hii ni tabia ya kila mwaka, watu wenye nafasi zao wanajipigia hela kama waliweka, lakini hakuna lolote linalofanywa.
Halafu tunajidanganya kuwa serikali inayoruhusu wizi wa mchana kama huu, inaweza kuisogeza mbele nchi yetu. Serikali ambayo haiwafungi wezi, inatetea ufisadi, tunaitegemea iboreshe huduma zetu za jamii. Ni lazima kwanza irejeshe fedha hizi zilizoibwa na watumishi wake ndipo tuitegemee kututendea haki tunayostahili!

No comments: