Moshi.
Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa
ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu
usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi
na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali
Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye
aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi
umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei
mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika
barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi
mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na
Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo,
lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF
linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna
haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia,
menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC
wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali
ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi
umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia simu ya
kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi
katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia
barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa
Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei
14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti
imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada
ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.
Pia,
kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo iahirishwe
kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa Mei 15.
Hata
hivyo, bado mhasibu huyo hajarejeshwa kazini na vikao vilikuwa
vinaendelea kuhusu hatua za kinidhamu zinazostahili dhidi yake.
“Wakati
hayo mambo mawili yanafanyiwa kazi, menejimenti imeamua kukusimamisha
kazi. Kabla hujaondoka unatakiwa ukabidhi vitendea kazi pamoja na simu
ya mkononi uliyokabidhiwa,” imedai.
Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema kwa nafasi yake, hawezi kulizungumzia.
Mhumba
alipotafutwa wiki iliyopita, alikiri kusimamishwa kazi kwa tuhuma za
kumtumia Rais ujumbe wa simu ya mkononi, ingawa alikanusha kuhusika.
“Maudhui
hayo kama ni kweli yalitumwa, hayana matatizo. Nimeongea na katibu mkuu
kumuuliza kama alipokea sms kutoka kwa Rais na kuwapa KCMC na namba ya
mtumaji amekanusha,” alidai.
Hata hivyo, alidai yeye
akiwa mwenyekiti wa Tughe, amekuwa akionekana kama adui pale anapojaribu
kutetea masilahi ya watumishi, likiwamo suala la kutopandishwa daraja
tangu mwaka 2007 hadi 2015.
“Ni kweli, watumishi
hawajapandishwa madaraja tangu 2007. Sisi (Tughe) tumekuwa tukilipigania
kwa sababu linachangia wastaafu kulipwa pensheni ndogo,” alisema.
“Mimi
kama kiongozi wa wafanyakazi, niko tayari kupeleka ushahidi kwa mambo
ambayo Tughe tumekuwa tukipambana nayo, ikiwamo mahali zilipo fedha za
mashine ya CT-Scan,” alisema Mhumba.
Tawi la Tughe
KCMC, limemwandikia barua katibu mkuu wa Tughe, ikiomba Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama aingilie kati suala hilo ili haki itendeke.
Gama alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupigiwa simu na Mhumba akimueleza lakini alimshauri aziandikie mamlaka husika.
Gama
alisema akiwa mwakilishi wa Rais mkoani Kilimanjaro, atachunguza nini
kimetokea baada ya kupata malalamiko rasmi kutoka kwa Mhumba au Tughe
yenyewe.
No comments:
Post a Comment