Waislam Watoa Tamko Zito Litakalosomwa Misikiti Yote Nchini......Wasema Wamechoka Kuonewa, Wawataka waamini wao Kufanya Maamuzi Magumu Wakati wa Uchaguzi - LEKULE

Breaking

8 Apr 2015

Waislam Watoa Tamko Zito Litakalosomwa Misikiti Yote Nchini......Wasema Wamechoka Kuonewa, Wawataka waamini wao Kufanya Maamuzi Magumu Wakati wa Uchaguzi



SIKU chache kupita baada ya Mkutano wa 19 wa Bunge kumalizika na serikali kuutupilia mbali mswaada wa sheria ambao unaruhusu kuwepo makakama ya Kadhi nchini, Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini wameibuka na kutoa tamko zito kwa kuwataka waislam wote nchini kutoshiriki kwenye kura ya maoni ya kupitisha katiba pendekezwa kwa madai kwamba serikali haina nia nzuri na waislam nchini kwa kitendo chake cha kukataa kuwepo mahakama ya Kadhi nchini.

Taasisi hiyo imewataka pia waislam wote kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura na kujiandaa kufanya uamuzi mgumu ambao wamesema haujawahi fanywa na waislam nchini tangu taifa hili lipate Uhuru.

Akisoma Tamko hilo lenye kura sita juzi jioni kwenye msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni Jijini Dar es Salaam ,Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislam nchini Sheikh Mussa Kundecha kwa niaba ya asasi za kiislam 11 zinazounda umoja huo na kushuhudiwa na Mamia ya waumini wa dini hiyo pamoja waandishi wa Habari alisema Waislam wamechoka na uonevu wanaodai kufanyiwa na Serikali iliyoko madarakani kwa kitendo cha kuondoa Mswaada wa Mahakama ya kadhi Bungeni ambapo alisema kitendo hicho ni kuendelea kuchochea vita ya kidini nchini.

“Kuna kila sababu ya kuamini kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kulishughulikia suala la mahakama ya Kadhi katika uhalisia wake kama ilivyoahidi kupitia ilani yake kwenye uchaguzi ibara ya 108 (b) mwaka 2005, na sasa inafanya hadaa za kisiasa kuwadanganya waislam ili waonekane wanalishughulikia suala la mahakama ya Kadhi kama walivyoahidi.

“Kwa ubabe huu wanaotufanyia waislam sasa tunawaomba waumini wote wa kiislam nchini kutoipigia kura katiba pendekezwa kwasababu sio katiba nzuri kwa waislam, halafu tunawataka kila mmoja aliyetimiza miaka 18 ajiandikishe kwenye Daftari wa wapiga kura ili kujiandaa kufanya uamuzi mgumu ambayo yatalitikisa taifa”. Alisema Sheikh Kundecha.

Alisema kuwa kitendo cha Serikali kuwatambua Makadhi wa Bakwata pamoja wanachosema ni ‘Mahakama hewa ya Kadhi’ chini ya Bakwata ni kinyume na Katiba ya nchini ibara 19(1) na (20) kwa kuwalazimisha waislam wawe chini ya Bakwata ambapo wanasema hawatakubaliana nalo.

Kuhusu Tamko la Maaskofu:
Pia katika Tamko la Taasisi hiyo ya kiislam ambalo litasomwa kila msikiti Ijumaa wiki hii nchi nzima, wamezungumzia Matamko mawili yaliyotolewa na Jukwaa la kikiristo nchini ambapo Taasisi hiyo ya Kiislam wameonyesha masikitiko yao kwa kusema ni dhahili hapa nchini kuna serikali dhaifu kwa kuwaacha maaskofu kutoa matamko ambayo wanadai ni ya kichochezi.

Kuhusu Kesi Za Masheikh na Kunyimwa Dhamana
Pia katika tamko hilo, waislamu wanadai kuchukizwa na kitendo cha Masheikh mbalimbali akiwemo shehe Ponda kunyimwa Dhamana na Serikali wakati Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Askofu Josephat Gwajima anaendelea kupeta uraiani

“Masheikh mbalimbali wako mahabusu, wamenyimwa Dhamana bila sababu za msingi kwa kesi za uchochezi au kwa kisingizio cha Ugaidi wakati huo huo tumeshuhudia Maaskofu wakitoa kauli za uchochezi pasina kuchukuliwa hatua yeyote ikiwemo sakata la Askofu Gwajima” alisema Kundecha

Kampeni Ya Kuua Madrasa
Pia Taasisi hiyo wamezungumia kitendo cha Serikali kuwakamata Mashehe mbalimbali wanaowafundisha watoto majumbani kwa madai ya serikali kutofuata taratibu za mafunzo likiwemo matukioa tofauti yaliyotokea mkoani Arusha. Katika tamko hilo wamedai ni wazi serikali imejitosa kuua madrasa nchini.

“Takriban mwezi mmoja sasa,njama za kuua madrasa zetu zimeibuka kwa kasi kubwa kwa kuendesha kamatakamata ya waalimu wa madrasa ambao hufundisha watoto Quran na mafunzo mengine ya Uislam majumbani mwao kama tulivyoshudia huko mkoan Moshi na Arusha”

“Tunataka Serikali itusaidie.Inaposema tufundishe Elimu ya dini ya Kiislam kwa mujibu wa sheria, Sheria hiyo ni ipi??? Ilipitishwa lini na Bunge lipi???

"Kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara 20 (1), kazi ya kutangaza dini ni suala binafsi,iweje sasa Serikali inakuja na madai haya ya kufundisha dini kinyume na Sheria kwa walimu wetu wa madrasa??" Alisema shehe huyo.

No comments: