Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema zaidi ya wabunge 50 wa vyama mbalimbali vya siasa nchini watajiunga na chama hicho kipya na kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Zitto ambaye alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana na kuzinduliwa mwezi uliopita.
Pia, amewatangazia vita wabunge wa majimbo manane ya Mkoa wa Kigoma, akijigamba kuwa ili waweze kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ni lazima wakubali kujiunga na ACT kwa kuwa chama hicho kimejipanga kuyabeba majimbo yote.
Akizungumza na Gazeti la Mwananchi jijini Dar es Salaam, Zitto alisema ACT ni chama kilichojipanga na ndiyo maana haikuwa ajabu katika mkutano wake mkuu wa hivi karibuni kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 400 na kufanya uzinduzi wa aina yake, huku akisisitiza kuwa chama hicho kinaungwa mkono na watu wengi.
“Tuna wagombea ubunge wengi wakiwamo wabunge wa sasa ambao katika Uchaguzi Mkuu Oktoba hawatagombea kupitia vyama vyao vya sasa. Wapo ambao hawatakwenda hata katika kura za maoni za vyama vyao na wameshafanya uamuzi,” alisema.
Huku akizungumza kwa kujiamini, Zitto alisema wabunge hao ndiyo sababu ya chama hicho kuwa na uwezo wa kujiendesha na kufafanua kuwa ACT kinawakaribisha wabunge na makada wote kutoka vyama vya Chadema na CCM.
“Wale ambao wanabanwa CCM na kukosa uhuru wa kuhoji jambo lolote hiki (ACT) ndicho chama chao. Wale ambao wanaamini kuwa aina za siasa tulizotaka kuzifanya ndani ya Chadema tukashindwa kuzifanya na wanadhani ni siasa muhimu zinazotakiwa, wapo na sisi,” alisema.
Kuhusu Kigoma
“Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba (Mbunge wa Kigoma Mjini-CCM) analijua. Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma lazima aje ACT,” alisema Zitto ambaye pia alirejea kauli yake kuwa atagombea ubunge katika jimbo jingine lakini siyo Kigoma Kaskazini.
Kauli hiyo ya Zitto inawagusa wabunge wa sasa wa majimbo ya Kigoma ambao ni; Felix Mkosamali (Muhambwe), Moses Machali (Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) na David Kafulila (Kigoma Kusini), wote wa NCCR-Mageuzi na Peter Serukamba (Kigoma Mjini, Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama (Manyovu) wa CCM.
Alipoulizwa iwapo wabunge hao wa majimbo ya mkoa huo ni miongoni mwa watu watakaohamia chama hicho alisema, “Sasa huo ni mtizamo wenu. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na msingi, nataka msingi uwe Kigoma.
"Tutakutana tena kwenye chumba hiki (cha mikutano) baadaye mwezi Novemba ili mnisute kwa kauli yangu na hapo itakuwa baada ya matokeo kutoka. Nahitaji kushinda kila kitu."
No comments:
Post a Comment