Uchaguzi waanza Sudan ,Upinzani unasusia - LEKULE

Breaking

13 Apr 2015

Uchaguzi waanza Sudan ,Upinzani unasusia



Uchaguzi mkuu nchini Sudan umeanza leo , huku Rais wa sasa Omar Al Bashir akitarajiwa kushinda.

Vyama vya upinzani vimesusia uchaguzi huu vikidai hautakua huru na wa haki.

Bashir ndiye kiongozi pekee wa nchi aliyewekewa waranti ya kukamatwa na mahakama ya kimataifa ya ICC.

Katika vituo vya kupigia kura wapiga kura wachache wamefika huko ilikutekeleza wajibu wao wa kikatiba.

Takriban wapiga kura milioni 13 watakuwa wakimchagua Rais na wabunge 450.

Matokeo yanatarajiwa kutangazwa Aprili 27.

Huu ndio utakaokuwa uchaguzi wa kwanza tangu Sudan Kusini ijitenge 2011.

Vyama vingi vya upinzani vinasusia uchaguzi huo kutokana na kile vinavyodai kuwa ukandamizaji wa kisiasa unaoendeshwa na rais Omar al Bashir.

Rais Bashir alifanya kampeni kubwa , akihutubia mikutano ya hadhara sehemu tofauti za taifa hilo kubwa.

Vyama vingi vya upinzani vinasusia uchaguzi huo ikiimanisha kuwa bashir na chama chake wana uhakika wa kushinda.

Wagombea 15 wanaoshindana na Bashir kwenye uchaguzi huo hawana uwezo mkubwa na wengine hata hawajulikani kote nchini Sudan.

Vyama vya upinzani vimesusia uchaguzi licha ya chama kimoja kikubwa kuwa na wagombea wa ubunge baada ya kudai kuwa itakuwa vigumu kwa uchaguzi huo kuwa wa haki.

Tangu mwaka uliopita wanasiasa kadha wa upinzani wamekamatwa huku vyombo vya habari vikiwekewa masharti makali.

Pia kuna mizozo katika majimbo la Darfur, Kordofan kusini na Bule Nile.

Nchi za magharibi zinaonekana kupendelea upinzani lakini rais Bashir ana matumaini kuwa ushindi wake utakubaliwa barani Afrika na kwenye nchi za kiarabu.

No comments: