UANDIKISHAJI KURA NI MTEGO, JINASUE! - LEKULE

Breaking

24 Apr 2015

UANDIKISHAJI KURA NI MTEGO, JINASUE!



UANDIKISHAJI Daftari la Kudumu la Kupigakura limeshakamilika katika Mkoa wa Njombe na habari nzuri ni kwamba vifaa zaidi vya kisasa vya BVR vimewasili, ili kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva ametuambia kuwa zoezi hilo lilichukua muda mrefu katika Mkoa wa Njombe kufuatia uchache wa vifaa na dosari nyingine ndogondogo, ikiwemo mashine hizo kutotambua vidole sugu, tatizo ambalo hata hivyo limesharekebishwa.

Kwa kumtazama Rais Jakaya Kikwete ambaye anaelekea katika miezi yake ya mwisho ya uongozi wa miaka kumi madarakani, ninayo imani kubwa kwamba kauli ya Tume juu ya kukamilika kwa zoezi hilo kwa wakati ni ya kuaminiwa na kwamba wananchi wanapaswa kuwaunga mkono watendaji wa tume watakaokuwa wakizunguka kote nchini kuifanya kazi hii.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura, ni moja kati ya vitu vichache ambavyo vinapata sapoti kutoka makundi yote ya kijamii Tanzania, iwe ni asasi za kiraia, kidini na hata vyama vya siasa. Kila mmoja kwa wakati wake, anawahimiza watu wake kuweka kipaumbele suala hili ili kuhakikisha hawakosi fursa ya kujiandikisha kwa vile kutofanya hivyo, ni kujipora haki yao ya kikatiba ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa mara zote ambazo makundi yote ya kijamii yameunga mkono jambo, hasa linaloonekana kuwa zuri kwa umma, hupata vikwazo kutoka kwa mamlaka, ambazo hufanya zinavyojua kupindua maana halisi ya mahitaji. Mfano mzuri tunaweza kuukuta katika mchakato wa katiba mpya.

Hakuna haja ya kurudia kusema kitu kilichokwishafanyika, lakini wote ni mashahidi wa jinsi matumaini makubwa ya wananchi yalivyoingia dosari baada ya rasimu iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kutekwa na kundi lenye itikadi moja, na hivyo kuondoa maana nzima ya kitu cha kitaifa kinachopatikana kwa maridhiano!

Ni kwa misingi hiyo, nina wasiwasi mkubwa na utendaji wa Tume ya Uchaguzi katika zoezi hili linalopigiwa debe na makundi yote. Uzoefu huu unanipa uoga kwamba huenda kukawa na vikwazo na visingizio visivyo na msingi ili kukwepa kuwaandikisha baadhi ya wapiga kura au hata kuharibu zoezi katika baadhi ya maeneo.

Kwa mfano, maeneo ya mijini yanaonekana kuwa na vijana wengi wanaoshabikia mabadiliko, kwa maana ya kuwa ni wafuasi wa upinzani. Na tunatambua kuwa demokrasia yetu, licha ya kuwa katika mfumo wa vyama vingi kwa zaidi ya miaka 20, bado watu wanaoshabikia upinzani wanaonekana kama maadui wa serikali.

Tume iweke mpango mzuri wa kuhakikisha haitengenezi mazingira ya vijana wa mijini kufanya fujo, kwa sababu kwenye malengo maalum, watu wenye akili zao wanaweza kutengeneza mazingira ya kuwapa watu hasira ili wafanye fujo. Hili likifanyika, vijana watakosa fursa yao muhimu na hivyo huenda ikasababisha hatari zaidi huko tuendako.

Labda niwaase pia vijana wa mijini. Pamoja na ujuaji wao na hamu yao kubwa ya kuona nchi inawasaidia kuboresha maisha yao, lazima watambue kuwa fujo zao, kwa namna yoyote ndiyo itakayowakosesha haki yao. Ni lazima wajue kuwa machoni mwa watu, wanaonekana kama wafanya vurugu wanaotumiwa na makundi yenye malengo maalum, wasikubali kuingia katika mtego huu.

Wafuate taratibu. Zoezi hili halitaki mwongozo wa vyama vya siasa wanavyoshabikia, isipokuwa maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mamlaka zitakazoteuliwa nayo, hivyo ni wajibu wao kusikiliza na kuzingatia bila kutoa nafasi ya kuharibu chochote.

Ni hadi hapo watakapofanikiwa kuwa na shahada ya kupiga kura, ndipo watakapoweza kumchagua diwani, mbunge na rais wamtakaye. Hili ni la msingi sana kulizingatia, vinginevyo, wataendelea kuwaruhusu watu kuwachagulia viongozi!]]

No comments: