MWAMUZI wa mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar, Stephen Makuka na msaidizi wake namba mbili Said Mnonga wameondolewa kwenye orodha za waamuzi wa Ligi Kuu na kufungiwa kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kushindwa kumudu mchezo huo.
Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambapo hata hivyo Kagera walikuwa walilalamikia bao la pili lililofungwa na Gaudence Mwaikimba kuwa lilikuwa lakuotea hivyo kuibuka vurugu uwanjani hapo kabla ya kutulizwa na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Kizuguto alisema timu ya Ruvu Shooting imepigwa faini ya Sh 300,000 kwa kosa la kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo katika mechi na Kagera Sugar iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Pia Maafande hao wamepigwa faini ya Sh 500,000 kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo.
Nayo Stand United imepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya mashabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa Polisi Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kizuguto alisema, Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi msaidizi namba moja Martin Mwalyanje na suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho hilo.
Alisema, kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh 500,000 kwa kumkanyaga na kutaka kumpiga mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi na Polisi.
Naye kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh 500,000 kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi.
Pia kamishna wa mechi hiyo, Bevin Kapufi amefungiwa mwaka mmoja kwa kutoa taarifa isiyo sahihi.
Naye kamishna wa mechi namba 159 kati ya Mbeya City na Simba, Joseph Mapunda amepewa onyo kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu huku Wekundu hao wa msimbazi wakilimwa faini ya Sh 300,000 kwa kosa la kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya Sh 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment