Ukisoma vitabu vya historia utaona kuwa nyayo za mtu wa zamani aliyeanza kutembea kwa miguu miwili zilipatikana katika Kijiji cha Endeluni, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kijiji hiki kipo kilometa 34 kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na eneo halisi lenye alama hizo za historia ya binadamu linajulikana kama Laetoli.
Tukiwa katika jopo la waandishi wa habari, tumewasili eneo la Laetoli ambalo kwa jamii ya Kimasai lina maana ya eneo lenye vitu vizuri, kwa kuwa lina bonde, miti na uwanda wa kupendeza wenye nyasi nzuri kwa ajili ya malisho ya mifugo ya nyumbani na wale wa porini na maji mengi kutoka Mto Ngarusi.
Tunapokewa na Simel Odorop (29) anajitambulisha kuwa yeye ni mlinzi mkazi wa Kijiji cha Enduleni. Anakiri kuwa pamoja na umaarufu wa eneo hilo, jamii haijanufaika kiuchumi kwa kuwa wageni hawafiki wengi, eneo hilo la kihistoria.
“Wageni hasa Wazungu wachache wanaokuja hapa wanataka kuona nyayo halisi lakini wakifika wanaonyeshwa kaburi zilimofikiwa. Wapo wanaotaka wafukue ili waone nyayo hizo, lakini tunawakataza,” anasema.
Anasema Serikali iliamua kuzifukia nyayo hizo ikisubiri ijengwe makumbusho ambayo itaweza kutunza vizuri nyayo hizo ili watalii wawe wanafika kuziona.
Godfrey Olle Moita ni mhifadhi wa mambo ya kale, anasema umaarufu wa eneo hilo utaongezeka mara mpango wa ujenzi wa makumbusho hiyo utakapokamilika.
“Eneo hili lina historia ya kipekee maana nyayo za Zamadamu Aferensis (Australopithecus Aferensis) watatu ziligundulika zenye umri wa miaka 3.6 milioni. Walishabihiana na binadamu wa sasa. Walitembea kwa miguu miwili wakiwa wima. Hii ni historia ya kipekee,” anasema.
Tangu nyayo hizo zimefukiwa, anasema ni miaka zaidi ya 20 imepita lakini baada ya ujenzi kukamilika zinaweza kufukuliwa na kuonekana vizuri bila kuathirika.
Anasema ufukiaji ulitumia mbinu za kitaalamu ambazo zinaweza kuzifanya zisiathirike kwa namna yeyote ile na zikifukuliwa zitaonekana kama zilivyogundulika. Nyayo ambazo zina umri wa miaka 20 tangu zimefukuliwa kisayansi ili mataifa mbalimbali yashuhudie maajabu hayo kabla ya kuzifukia mwaka 1998 miaka 17 iliyopita.
Anasema maajabu hayo ni kivutio kikubwa cha utalii ambacho kwa miaka zaidi ya 37 kilikuwa chini ya Mambo ya Kale, kikitumika kama sehemu ya utafiti.
Kwa sasa, anasema kimehamishiwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kinapaswa kutangazwa kama kivutio cha utalii wa kipekee.
Ziligunduliwaje
Mwaka 1976, Andrew Hill na David Western, watafiti washiriki kwenye timu ya Dk Mary Leakey wakiwa Laetoli baada ya kumaliza kazi wakawa wanacheza huku wanatupiana kinyesi kikavu cha tembo.
Dk Hill alipoangalia chini aligundua alama zilizokuwa kwenye mwamba, ndipo mwaka 1978 Dk Paul Abell aligundua zilikuwa nyayo za binadamu wa kale. Uchunguzi wa kihistoria ukabaini kuwa ni nyayo za binadamu wa kale ajulikanaye kama Zamadamu ambaye alitembea wima kwa miaka milioni 3.6.
Kabla ya hapo inaaminika kuwa binadamu alikuwa anatembea kwa miguu na mikono, kama ilivyo wanyama.
Changamoto zinazowakabili
Anasema kuwa mmomonyoko unaosababishwa na maji, upepo na uzito wa udongo katika eneo hilo ni miongoni mwa mambo ambayo wanahisi yanaweza kusababisha alama hizo za kale kuathirika. Mambo mengine anasema ni wadududu wanaochimba ardhi kama vile panya wanaweza kuathiri pamoja na mizizi ya mimea katika eneo hilo ambalo zilifukiwa futi tano kwa udongo.
Hali ya hewa ya joto na baridi vinaweza kuathiri hali ya udongo hivyo alama kupotea au kupoteza uhalisia.
Wageni wachache kufika eneo hilo
“Tunapata wageni wachache sana wanaokuja hapa licha ya umaarufu huu, hasa wanatoka Marekani ambako mgunduzi alitokea, lakini kila anayefika, hurejea kwao akiwa hana furaha kwa sababu hatekelezi kiu yake.
Kinachowaudhi ni kwamba licha ya kulipia, hawaoni kitu halisi bali eneo ambalo alama hizo zimefukiwa na katika hali ya kutoridhika huomba kama kuna uwezekano zifukuliwe ili baada ya kuziona, zifukiwe.
Siyo wageni tu ambao hupata adha hiyo bali hata wanafunzi hapa nchini ambao hufika eneo hilo ili wajifunze mambo ya historia ambayo wameyasoma vitabuni.
Kutokana na hali hiyo, watalii wengi hukata tamaa ya kufika maeneo hayo na hasa ikizingatiwa kuwa baada ya kutoka nchini huwaeleza wenzao hali halisi.
Hii ni kusema watalii wengi ambao wangeweza kufika nchini ili kuona maajabu hayo ya kihistoria, wanashindwa kuja kwa sababu tu wamepata habari kuwa nyayo hizo kwa sasa zimezikwa ardhini.
Hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhimiza ujenzi wa makumbusho hayo, ili kuongeza mapato ya Serikali yanayotokana na utalii.
No comments:
Post a Comment