SUMATRA YASEMA LAZIMA NAULI ISHUKE - LEKULE

Breaking

2 Apr 2015

SUMATRA YASEMA LAZIMA NAULI ISHUKE



Meneja Mawasiliano wa SUMATRA, David Mziray

SIKU chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kutaka uangaliwe uwezekano wa kushusha nauli za vyombo vya usafiri nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema inatekeleza agizo hilo na kwamba nauli za daladala na mabasi ya mikoani zitashuka wakati wowote kuanzia sasa.

Imeongeza kuwa, licha ya bei ya mafuta kupanda kidogo jana, hakutaathiri kushuka kwa nauli, kwani ukokotoaji utafanyika kwa wastani wa bei ya mafuta ilivyoshuka kwani haitapanda kwa kiasi kikubwa kwa mara moja.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, David Mziray aliyesema wanatekeleza agizo la Waziri Sitta aliyetaka nauli zishuke kufikia kesho, lakini wamechelewa kutokana na muda wa kuwasilisha maoni kwa wadau waliopewa siku 14 kufikia ukomo leo.

“Tunawahakikishia wananchi kuwa baada ya kumaliza siku za kupokea maoni ya wadau hususan wamiliki wa mabasi ya daladala waliopewa siku 14, mchakato huu utakwenda haraka na mapema iwezekanavyo tutatangaza nauli hizo mpya,” alisema.

Mziray alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kutoshusha nauli, bali wanafuata taratibu na kanuni hivyo kuwataka wananchi kuwa na subira kwa siku chache zijazo.

Wiki hii, Waziri Sitta aliwataka Sumatra kuharakisha mchakato huo wa kushusha nauli ufanyike haraka iwezekanavyo na ifikapo kesho wawe wametangaza nauli hizo mpya, kwani kwa muda mrefu bei za mafuta zimeshuka kutoka zaidi ya sh 2,200 hadi chini ya Sh 1,800.

Wadau wa usafiri walipendekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa kilometa 10.

Walitaka kwa mabasi ya kawaida kwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya Sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh 16,700).

Kwa usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa kuwa Sh 31.39 kwa usafiri wa kilometa 10 badala ya Sh 400.

No comments: