Sherehe za Miaka 51 ya Muungano: Vikosi Vya Ulinzi Vyafanyiwa Maboresho...... Mtu Mmoja Akamatwa na Wanajeshi Kwa Kujifanya Usalama wa Taifa - LEKULE

Breaking

27 Apr 2015

Sherehe za Miaka 51 ya Muungano: Vikosi Vya Ulinzi Vyafanyiwa Maboresho...... Mtu Mmoja Akamatwa na Wanajeshi Kwa Kujifanya Usalama wa Taifa


Baada ya Rais Kikwete kuingia alipokelewa na Mkuu ya Jeshi la Wananchi(JTWZ),Generali Davis Mwamunyange ambaye alimpeleka kukagua vikosi vya ulinzi na usalama.

Jeshi hilo limeonekana kufanya maboresho katika gwaride la mwaka huu ambapo waliandaa gadi 20 huku gadi 13 zikiwa nje ya uwanja na gadi 7 zikiwa ndani.

Gadi 13 zilizokuwa nje ya uwanja zilivalia mavazi ya mazoezi (Combat)huku wakiwa wamebeba vifaa vya kivita ambapo kati ya hizo,gadi 1 ilikuwa kikosi maalum cha makomandoo na gadi iliyobaki ilikuwa kikosi maalum cha wanamaji.

Gadi saba zilizobaki ndani kikiwamo na kikundi cha bendi walikuwa wamevaa mavazi rasmi ya gwaride.

Baada ya rais Kikwete kuingia ndani alipokelewa na Mkuu wa Majeshi(CDF), Davis Mwamunyange ambaye alimpeleka kukagua gadi saba zilizokuwa ndani huku mizinga 21 ikilia.

Baada ya kukagua, gadi hizo zilisogea mbele kwa hatua 15 kwa ajili ya kutoa heshima zao kwa amiri jeshi mkuu na kuendelea kusimama ndani ya uwanja huku wakisubili gadi zilizokuwa nje ziweze kupita mbele ya amiri jeshi.

Gadi 11 zilipita kwa mwendo wa pole huku gadi mbili moja ikiwa kikosi cha makomandoo na wanamaji zilipita kwa mwendo wa kasi.

Viongozi Wanena:
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maadhimisho hayo, baadhi ya viongozi wakuu wastaafu wa serikali walisema kuwa muungano huo unapaswa kuigwa na mataifa mbalimbali.

Spika Mstaafu Pius Msekwa alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuuenzi na kuendeleza muungano huo ili uweze kudumu miaka hamsini mingine.

“Sisi tumestaafu, tunawaachia vijana ili waweze kuendeleza, hivyo basi wanapaswa kuunga mkono na kuudumisha ili uweze kudumu miaka mia moja,”alisema Spika Mstaafu Pius Msekwa.

Alisema licha ya muungano huo kupitia kwenye mawimbi yaliyoibua kero za muungano, mpaka sasa wameweza kuyashughulikia na kubakisha mambo machache ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi.

Akitolea mfano wa baadhi ya nchi ikiwamo Gambia na Senegal ambazo zilishindwa kudumisha muungano baada ya kujitokeza kwa migogoro ya hapa na pale.

Msekwa alisema kuwa ili kuonyesha kuwa muungano ni jambo la muhimu, ametunga kitabu maalum ambacho kimeelezea mambo mbalimbali yanayohusu muungano na misingi imara ya kuuenzi.

Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema kuwa, muungano huo umeweza kuleta mafaniko makubwa katika Nyanja mbalimbali ikiwamo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema hivyo basi wanapaswa kuuenzi na kuudumisha ili uweze kudumu miaka hamsini ijayo.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, vijana wengi wanapaswa kujitokeza ili waweze kujiandikisha na kupiga kura.

“Ushiriki wa vijana kwenye kupiga kura kwa ajili ya katiba inayopendekezwa ni muhimu, kwa sababu inaweza kusaidia katika uchaguzi mkuu,”alisema Butiku.

Mtu Mmoja Akamatwa
Mtu mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikamatwa na wanajeshi kwa kujifanya ni afisa wa usalama wa taifa.

Kijana huyo ambaye alionekana katika maeneo hayo akiwaongoza wananchi ili waweze kuingia ndani ya uwanja alikamatwa baada ya kubainika kuwa ni afisa feki wa usalama.

Baada ya kuhojiwa ilibainika kuwa aliwahi kuwa Askari wa Jeshi la Wananchi na kufukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu, jambo ambalo liliwafanya maofisa hao kumpeleka kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya mahojiano zaidi.

No comments: