STRAIKA Mtanzania, Mbwana Samatta, juzi Jumamosi alipatwa na janga kubwa, baada ya kupigwa na jiwe kisogoni na kupasuka sehemu hiyo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya DR Congo uliozikutanisha TP Mazembe na Shark XI FC kwenye Uwanja wa Tata Raphael jijini Kinshasa nchini humo.
Mchezo huo uliomalizika kwa TP Mazembe kupoteza kwa mabao 2-1, ulikumbwa na vurugu kwa muda wote hali iliyoufanya mchezo huo kusimama mara kwa mara.Akizungumza moja kwa moja kutoka DR Congo, Samatta alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa anaendelea vizuri baada ya kutokea ajali hiyo ambayo aliipata mara tu mchezo ulipomalizika.
“Namshukuru Mungu kwa sasa naendelea vizuri, hali ya mchezo wetu ilikumbwa na vurugu nyingi zilizotokana na mashabiki kurusha mawe uwanjani na kusababisha mwamuzi kuusimamisha mara kwa mara, kiukweli ilikuwa hatari na kutufanya tupoteze umakini uwanjani.
“Nilishtuka nilipopigwa na jiwe kichwani na nilipogusa niliona damu zikinitoka lakini sijashonwa kutokana na jeraha lenyewe kuwa dogo na badala yake nimesafishwa tu,” alisema Samatta.
No comments:
Post a Comment