Sakata la Gwajima: Polisi Wamhoji Kwa Masaa Matano..... Atakiwa Kurudi Polisi Wiki Ijayo na Hati ya Usajili wa Kanisa Lake,Helkopta na Viwanja Anavyomiliki - LEKULE

Breaking

10 Apr 2015

Sakata la Gwajima: Polisi Wamhoji Kwa Masaa Matano..... Atakiwa Kurudi Polisi Wiki Ijayo na Hati ya Usajili wa Kanisa Lake,Helkopta na Viwanja Anavyomiliki



Askofu wa Kanisa la Ufufua na Uzima Josephat Gwajima amelitikisa tena Jiji la Dar es Salaam jana mara baada kuwasili makao makuu ya Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ili kuendela na mahojiano kuhusu tuhuma za kumkashfu Askofu Pengo.

Gwajima aliwasili Makao Makuu ya Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Majira ya saa mbili kamili asubuhi huku akisindikizwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa la Ufufuo na Uzama pamoja na Mwanasheria wake .

Eneo lote la kituo hicho cha polisi lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa mbalimbali wa Usalama wa Taifa wakisaidiwa na Jeshi la Polisi.

Baada ya kuwasili kituoni hapo, umati mkubwa wa Waumini wake ulizunguka maeneo yote ya Kituo hicho huku wengine wakiwa maeneo ya stendi ya Treni ya Reli ya kati.

Kama kawaida, Waumini hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali ambazo wanadai zilikuwa mahususi kumpa nguvu Askofu huyo ajibu kesi hiyo kwa ufasaha.

Baada ya Mahojiano ya takribani masaa Matano, hatimaye Askofu Gwajima alitoka ndani ya kituo hicho,lakini katika hali isiyo ya kawaida,Askofu huyo aligoma kuongea na vyombo vya habari.

Baada ya Gwajima kugoma kuongea,mwandishi wetu alimfuata Mwanasheria wake aliyekuwa ameambatana naye,John Mallya ambaye alisema kuwa mteja wake alikuwa amechoka, hivyo asingeweza kuongea.

Mallya alimweleza mwandishi kuwa mambo aliyohojiwa Gwajima ni kuhusu mali zake na sio matamshi ya kumtukana Askofu Pengo.

“Mahojiano yamekwenda vizuri lakini nasikitika sana kutokana na mambo waliyokuwa wanamhoji. Wamemuuliza mambo ambayo hayahusiani kabisa na kile tulichotarajia na ndicho kilichotuleta hapa, nilidhani mteja wangu ataulizwa kuhusiana na matumizi ya lugha chafu iliyodaiwa kutumika kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini,” alihoji wakili wa Gwajima.

Aliendelea kusema kuwa, mambo aliyoulizwa ni kuhusiana na ukoo wake, wazazi wake hata ndugu zake na watu wengine wa kwao waliokufa.

Alisema walihoji pia juu ya mambo mengine kama umiliki wa helikopta, utajiri wake, nyumba anayoishi, uhusiano wake na watu mbalimbali.

“Nimeshangaa sana kuona mteja wangu ameulizwa vitu kama hivyo ambavyo havihusiani na madai ya hapo awali ya matumizi ya lugha ya matusi. Tumeagizwa tulete nyaraka kumi siku ya mahojiano yetu tena yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu na sisi tutafanya hivyo,” alisema Mallya.

Alizitaja nyaraka na vitu vingine wanavyotakiwa kuvipeleka Aprili 16 ni hati ya usajili wa kanisa, bodi ya udhamini wa kanisa na majina yao, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake, na muundo wa uongozi wa kanisa lake.

Vingine ni namba ya usajili wa kanisa, ritani za kanisa lake (mapato na matumizi ya fedha za kanisa lake), mtu anayechukua na kurekodi mkanda wa video kanisani kwake, pamoja na waraka wa Baraza la Maaskofu uliosomwa makanisani.

No comments: