Shahidi wa nne katika kesi ya tuhuma za ubakaji inayomkabili Emmanuel Mbasha, mume wa mwanamuziki wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, jana alidai mahakamani kuwa hakuona dalili zozote za kuingiliwa kimwili mlalamikaji.
Hayo yalidaiwa na daktari wa Hospitali ya Amana, Migole Mtuka, ambaye alimfanyia vipimo msichana huyo.
Daktari huyo alidai katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwamba vipimo alivyomfanyia msichana huyo anayedaiwa kubakwa na Mbasha, havikuonyesha kitu chochote.
Dk. Migole alidai kuwa binti huyo alifika hospitalini hapo Mei 26, mwaka jana, kwa alili ya kufanyiwa vipimo.
Alidai kwamba binti huyo alipofika hospitalini hapo, alimfanyia kwanza vipimo vya macho kisha kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, ambavyo hutolewa bure.
Dk. Migole alidai kwamba baada ya kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, akiwa na baadhi ya ndugu wa familia yake, hakwenda bali aliingia mitini na kurejea Juni 3, mwaka jana, baada siku nane kupita.
Alidai baada ya kufanyiwa hivyo, vipimo hivyo vilionyesha kuwa hakuna kitu chochote alichofanyiwa, kwa maana ya kubakwa au kuingiliwa na mwanamume katika mwili wake na kuwajazia fomu aina ya PF3 kwa kile alichokiona.
“Binti huyo hakuonekana kuwa na ujauzito, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na wala mbegu za kiume katika sehemu za siri,” alidai daktari huyo.
Hata hivyo, baada ya kutolewa ushahidi huo, Hakimu Flora Mujaya, hawakuweza kusikiliza ushahidi mwingine kutokana na taarifa za msiba wa hakimu mwenzao, zilizofika mahakamani hapo.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa upande wa Jamhuri Aprili 20, mwaka huu.
Mbasha anadaiwa kuwa Mei 23 na 25, mwaka jana, alimbaka binti mwenye umri wa miaka 17, ambaye anadaiwa ni shemeji yake huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment