Kuyumba na hatimaye kupeperuka kwa Kura ya Maoni kwa Katiba Inayopendekezwa kulianza kama mzaha pale kila kiongozi alipotoa tamko lililokinzana na mwingine.
Kwanza ni kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba anatamani Kura ya Maoni ipigwe siku ya Uchaguzi Mkuu.
Alisema hayo Oktoba 2014 lilipoahirishwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) lililokuwa limejaa wajumbe wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pili ni kauli iliyotolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwamba Kura ya Maoni itafanyika Machi 30, 2015.
Tatu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva abainisha kwamba kura ya maoni haiwezi kufanyika Machi 30 kwa sababu kazi ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura haitakuwa imekamilika.
Nne, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ziarani nchini China, mwaka jana alisema kwamba Kura ya Maoni itafanyika Aprili 30, 2015.
Matamko hayo yaliwachanganya wananchi, kwani hata Rais Kikwete mwenyewe alikuwa hajawaambia Watanzania kuhusu tarehe hiyo isipokuwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini China.
Kutolewa kwa matamko tofauti kuhusiana na Kura ya Maoni zilikuwa dalili tosha kwamba Serikali haikuwa imejiandaa na kutoka na kauli moja inayoeleweka.
Matokeo yake Watanzania wamepoteza muda mwingi kwa jambo ambalo hatimaye limekwama.
Je, nani alaumiwe? Tume au Serikali? Je, upo uwezekano sasa wa Kura ya Maoni kufanyika siku moja na Uchaguzi Mkuu kama alivyotamani Pinda?
Usimamizi wake ukoje?
Tume ina uwezo wa kusimamia mambo mawili hayo kwa wakati mmoja?
Haya ni baadhi ya maswali ya msingi kabisa kujiuliza ili kutegua kitendawili cha hatima ya Kura ya Maoni.
Wapo wanaopeleka lawama moja kwa moja kwa Nec iliyopewa jukumu la kuandikisha wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR).
Nec katika mipango yao waliomba wapewe fedha za kununua mashine 15,000 ili waweze kutekeleza wajibu huo kwa muda mfupi, lakini Serikali ikawaahidi kuwapa fedha za kununulia mashine 8,000.
Hadi leo haijapewa fedha za kununua mashine hizo. Kama hivyo, ndivyo, kwa nini Nec ibebeshwe lawama kwa makosa ya Serikali?
Hapa Serikali haiwezi kujiweka kando na lawama za kukwama kwa zoezi hilo kwani yenyewe ndiyo inayopaswa kuiwezesha Nec kwa hali na mali kuweza kutimiza mipango yake.
Kilichokwamisha
Imekuwepo hali ya kutoaminiana kati ya vyama vya siasa tangu wakati wa uundwaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2011. Chama tawala, CCM, kilikuwa kinavutia upande wake na vyama vya upinzani vilikuwa vinaangalia upande wao.
Mara kadhaa vyama vya upinzani vilitoka nje ya Bunge kupinga baadhi ya vipengere na kutokana na nia njema aliyokuwa nayo Rais Kikwete aliwaita Ikulu na wakamaliza tofauti baina yao. Pili, Rais Kikwete alipenda kusikiliza matakwa ya CCM.
Alipokutana na viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD), alitoa mwelekeo mzuri lakini alipokutana na chama chake alitoa kauli tofauti.
Mfano ni katika vikao na TCD walikubaliana Kura ya Maoni iahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, lakini alipokutana na viongozi wa CCM aliruhusu “ngoma” iendelee.
Mfano mwingine ni namna Rais Kikwete alivyoteua wajumbe kwa kuzingatia ufuasi wao na si uwezo, wengi wakiwa wanaCCM.
Hila zatawala
Mambo mengi yalifanyika kwa hila. Kwanza, ni pale wafuasi wa CCM walipobadilisha sheria kuzuia wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Jaji Joseph Warioba kuwa miongoni wa wajumbe wa BMK.
Hali hii ilileta manung’uniko makubwa kutoka kwa wadau ambao walijua umuhimu wa tume ile kuwa sehemu ya Bunge la Katiba kwani ndiyo iliyopita nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi.
Pili, ni kuvurugwa kwa kanuni zilizotungwa na BMK. Kanuni zilitaka Rais Kikwete azindue BMK ndipo siku inayofuata aitwe Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu Warioba asome Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba hadi atakapomaliza.Hata hivyo, walifanya hila, Warioba aliitwa kusoma Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba ndipo akaalikwa Rais Kikwete ambaye aliichanachana Rasimu iliyoandaliwa, huku akisoma Mapendekezo ya CCM yenye kitu kilichoitwa Muungano ulioboreshwa.
Kwa hatua ya Rais kupuuza Rasimu ya Warioba iliyotokana na maoni ya wananchi, wapinzani waliungana na kuwa na sauti ya pamoja ya kupinga kila kilichokuwa kikiendelea ndani ya BMK na ndipo Aprili 16, 2014 wakasusia. Ushirikiano wa kusuia BMK ndiyo uliwapa nguvu na kuunda umoja uitwao Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Tatu, mchakato huo uliendelea kuingia doa pale Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar walipojitoa kuwa sehemu ya Katiba ile.
Ikumbukwe, wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman alipinga waziwazi baadhi ya vifungu vilivyopo katika Katiba pendekezwa, Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar Abubakary Khamis Bakary yeye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Ukawa waliosusia vikao.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu
Uchaguzi Mkuu huu, moja ya maswali niliyouliza hapo juu ni je, upo uwezekano sasa wa Kura ya Maoni kufanyika siku moja na Uchaguzi Mkuu kama alivyotamani Pinda.
Swali hili ni muhimu wananchi wakaendelea kuuliza kutokana na kauli tata za viongozi wa Serikali; bado wapo wanaolazimisha Kura ya Maoni ifanyike katika mazingira yoyote. Sawa, lakini lini?Tangu Februari 23, Nec inahangaika kuandikisha wapigakura wa Mkoa wa Njombe pekee. Itawachukua miezi mingapi kuandikisha nchi nzima? Kwa mwenendo huu wa konono ipo hatari siyo tu ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu kufanyika siku moja, bali vyote viwili kutofanyika kabisa.
Wakati akili na nguvu za vyama vya siasa iko kwenye uchaguzi mkuu, Nec haina uhakika wa kupewa vifaa vyote 8,000 ili ikamilishe kazi ya uandikishaji wa wapigakura kwa muda na ipate muda wa kuhakiki majina.
Hatari ya mambo mawili hayo kutofanyika ni kutokana na kauli ya Lubuva kwamba “hakuna uchaguzi mkuu ikiwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura utakuwa haujakamilika?” Je, kazi hiyo itakamilika lini.
Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema endapo hakutakuwa na umakini na juhudi za makusudi kusimamia zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, huenda uchaguzi mkuu nao usifanyike mwezi Oktoba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo anasema ukiachilia mbali kasoro lukuki zilizojitokeza katika mchakato wa kura za maoni, maandalizi hafifu ya uandikishaji daftari la wapigakura nayo yamekuwa sehemu ya changamoto.
Dk Makulilo anasema kama hali ya uandikishaji itaenda kwa kusuasua kama ilivyotokea katika Mkoa wa Njombe, ipo hatari ya kushindwa kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
“Tusipojiandaa vizuri hata huo Uchaguzi Mkuu wanaweza kusogeza mbele na hili likitokea litakuwa na madhara makubwa kwa taifa kwani hapo unazungumza kwamba Rais aendelee kukaa madarakani kwa muda zaidi na hii inapaswa kuidhinishwa kikatiba” anasema. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho anasema endapo Serikali haitaweka bayana kuahirisha suala la Kura ya maoni kufanyika mwaka huu, haoni uwezekano wa kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
“Ili tuweze kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Serikali itangaze wazi kuwa hakutakuwapo na Kura ya Maoni ya Katiba…Tusiyachangaye mambo haya mawili na vinginevyo tuiongezee Serikali muda kwa mujibu wa sheria inavyopaswa maana sioni kufanikiwa mambo haya yakienda pamoja,” anasema Shumbusho.
Anasema muda uliobaki, haiwezekani Serikali ikaendesha mambo yote mawili. “Endapo italazimisha kubeba Uchaguzi Mkuu na kura za maoni itabidi Serikali iongezewe muda zaidi ili nguvu zielekezwe kwenye Kura ya Maoni.
No comments:
Post a Comment