Mwanamuziki Percy Sledge aaga dunia - LEKULE

Breaking

15 Apr 2015

Mwanamuziki Percy Sledge aaga dunia


Mwanamuziki chapa 'Soul' aliyetikisa ulimwengu kwa miaka mingi kutokana na utunzi wake ''When a Man Loves a Woman'',Percy Sledge ameaga dunia.

Raia huyo wa Marekani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 nyumbani kwake Baton Rouge, Louisiana.

Afisa wa muungano wa wasanii Steve Green, ameithibitishia BBC kifo cha muimbaji huyo nguli.

Wimbo wake uliovuma kote duniani kwa miaka na mikaka '' When a Man Loves a Woman'' uligonga orodha ya kumi bora mara mbili nchini Uingereza.

Sledge aliyewahi kuvuma katika runinga ya BBC Two mwaka wa 1994 kwa ushirikiano na Jools Holland alishikilia nafasi ya kwanza kwa majuma mawili mfululizo alipozindua wimbo huo''When a Man Loves a Woman'' mwaka wa 1966.

Muimbaji huyo pia alitesa sana nchini Uingereza wimbo wake huo ulipopanda hadi nafasi ya nne katika jedwali la kumi bora.

Na haikuishia hapo Percy Sledge, alirejea kwa kishindo mwaka wa 1987 alipotoa nakala ya wimbo huo na mara utunzi wake ukabobea kwa mara nyengine tena nchini Uingereza.

Wimbo huo ''When a Man Loves a Woman'' ulivuma na kuwa wapili kwa umaarufu nchini Uingereza.

Sledge alisherehekea miaka 49 tangu alipotangazia ulimwengu wa Muziki wa Soul kuwasili kwake na wimbo huo ''When a Man Loves a Woman''.

Bwana huyo aliweka historia alipoandikwa katika daftari la wanamuziki waliobobea yaani '' Rock and Roll Hall of Fame katika mwaka wa 2005''.

Sledge alikuwa mwanachama wa muungano wa wanamuziki kutoka Alabama.

Sledge aliwahi kuwa muuguzi kabla ya kufuata talanta yake na kuibukia kuwa muimbaji hodari.

Mbali na wimbo wake maarufu ''When a Man Loves a Woman'' Sledge pia anakumbukwa kwa tungo zake kama ''Warm and Tender Love'


''It Tears Me Up'' na ''Take Time to Know Her''.

Wimbo wake ''When a Man Loves a Woman' ulipata umaarufu zaidi mwaka wa 1991 baada ya msanii hodari Michael Bolton kutoa chapa ya wimbo huo na ukagonga kilele cha orodha ya nyimbo maarufuzaidi duniani.

Chapa ya sledge hata hivyo ndio iliyokuwa wimbo wa kwanza uliorekodiwa katika studio za Alabama za Muscle Shoals uliwahi kuwa nambari moja duniani..

Studio hizo za Alabama ndizo zilizotumika kwa kuwanakili wasanii shupavu Aretha Franklin na kundi la the Rolling Stones .

Vilevile wimbo wa''When a Man Loves a Woman'' ndio uliokuwa wa kwanza kupigwa chapa ya dhahabu yaani wimbo uliopendwa sana kote duniani kuwahi kurekodiwa chini ya nembo ya Atlantic.

No comments: