Muswada wa Mahakama ya Kadhi Waondolewa.....Hautawasilishwa Bungeni LEO. - LEKULE

Breaking

1 Apr 2015

Muswada wa Mahakama ya Kadhi Waondolewa.....Hautawasilishwa Bungeni LEO.



Muswada wa Mahakama ya Kadhi umeondolewa bungeni na sasa hautajadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge unaohitimishwa leo mjini Dodoma.

Huu ni muswada wa tatu kuondolewa Bungeni baada ya ile miwili ya sekta ya habari ambayo ni muswada wa Sheria ya kupata Taarifa wa mwaka 2015 na ule wa sheria ya huduma wa Vyombo vya Habari iliyoondelewa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Muswada huo ulipangwa kuwasilishwa Bungeni leo, lakini serikali imeamua kuuondoa kutokana na hofu ya kutokea mpasuko nchini.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, akizungumza na mwandishi wetu jana ofisini kwake alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautakuwapo tena katika mkutano huo.

Dk. Kashilila alisema haijulikani ni lini utawasilishwa bungeni kwa sababu Mkutano wa Bunge ujao unaotarajia kufanyika Mei, utakuwa mahsusi kwa ajili ya bajeti.

“Waziri Mkuu alivyosema wataangalia na kushauriana kimsingi, alitoa maneno ya busara tu au ilikuwa kauli ya mtu mzima, lakini huu muswada hautakuwapo,” alisema.

Dk. Kashilila alisema hali iliyojitokeza Jumapili iliyopita wakati wa semina ya wabunge haikuwa nzuri kutokana na mvutano mkali miongoni mwa wabunge.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipoulizwa kuhusu kama muswada huo utawasilishwa bungeni, alisema hakuwa na majibu badala yake alitaka suala hilo iulizwe ofisi ya Spika.

“Suala hili usiniulize, nenda Ofisi ya Spika au muulize huyu (Magati) ambaye yupo sekretarieti,” alisema huku akiwa na haraka kuelekea ofisini kwake.

Naibu Spika, Job Ndugai, akizungumza na mwandishi nje ya ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya kuahirisha Bunge, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautawasilishwa bungeni leo.

“Huo muswada hauwezi kuletwa bungeni kutokana na hali ilivyo,” alisema Ndugai bila kufafanua zaidi.

Naye Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro, alipoulizwa kama muswada huo utawasilishwa bungeni alimtaka mwandishi asimuulize maswali yanayohusiana na muswada wa Mahakama ya Kadhi.

“Sitaki kabisa kuulizwa suala la Muswada wa Mahakama ya Kadhi, “alijibu Dk. Migiro kwa hasira huku akiingia kantini.

Tujikumbushe
Februari mwaka huu, muswada huo pia uliondolewa bungeni kwa kile Mwanasheria Mkuu wa Serikali alichodai kwamba ni kwenda kuonana na viongozi wa dini kuwaelemisha juu ya mahakama hiyo, ili uwasilishwe tena kwenye mkutano unamalizika leo.

Mwishoni mwa wiki nusura wabunge wazipige kavu kavu huku wakirushiana maneno wakati wa semina kuhusu Mahakama ya Kadhi.

Kutokana na joto lilivyopanda, baadhi waliamua kususia semina hiyo na kutoka huku wengine wakibaki na kurushiana vijembe. Semina hiyo iliandaliwa na Bunge.

No comments: