MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amevionya vyama vya siasa na wanasiasa wasikamiane na kukomoana kwa sababu, kufanya hivyo hakujengi demokrasia wala kuisaidia nchi.
Badala yake, amevielekeza viimarishe uelewano na kusaidiana, ili kujenga Tanzania yenye amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kufungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano ya jinsi ya kufikia na kuutekeleza uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa amani, Jaji Mutungi alisema ameona dalili za wanasiasa na vyama vyao kukamiana.
Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), litakalotoa ripoti ya utendaji wa ofisi hiyo katika mkutano utakaoendelea leo jijini humo, lengo likiwa kuishauri namna ya kuboresha utendaji.
Katika mkutano huo unaohusisha wadau mbalimbali wa siasa nchini, wakiwemo wawakilishi wa vyama 22 vya siasa na taasisi tofauti, Jaji Mutungi alisema, “Tanzania ina tunu ya amani, hivyo wanasiasa wasijaribu kuivuruga kwa kuendesha siasa zisizo zingatia dhana ya demokrasia ya kweli."
Alionya kuwa uzembe wowote utakaofanywa na wanasiasa au vyama vyao unaweza kuiathiri nchi, na kuwafanya Watanzania wajute kuingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi.
Jaji huyo alisema pia kuwa amejiridhisha kuwa baadhi ya vyama vya siasa vimeshindwa kuielewa vizuri dhana ya demokrasia ya vyama vingi, hivyo kuwa na fikra za kukamiana na kukomoana, ambazo kwa namna yoyote, hazimsaidii Mtanzania.
“Ninawaomba wanasiasa na vyama vyenu muelewe kuwa, harakati zote za kufikia uchaguzi mkuu zinapaswa kuwa na lengo la kumtafuta kiongozi atakayeiendesha nchi ifikie maendeleo.
“...Sote tunajenga nyumba moja ambayo ni nchi yetu, hivyo, hatupaswi kugombania fito kwa mtindo utakaosababisha nyumba isijengwe,”Jaji Mutungi alisisitiza na kuongeza kuwa mikutano kama hiyo itaendelea kuwepo ili kupanua uelewa wa wanasiasa juu ya dhana hiyo ya demokrasia ya vyama vingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Philipe Poinsot aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kukuza demokrasia ya vyama vingi na kuwakumbusha wanasiasa na vyama vyao kuwa wao ndio wenye dhamana ya kuilinda demokrasia hiyo pamoja na amani iliyopo.
Alisema,”katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, Tanzania imekuwa na vuguvugu linaloweza kusababisha hali ya sintofahamu kwa wananchi, jambo ambalo si jema hasa endapo nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu na matukio muhimu ya upigaji kura ya maoni."
Katika hatua nyingine, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa, Dk Benson Bana alisema, ingawa demokrasia ya vyama vingi inaonesha kuanza kufanikiwa nchini, vyama vya siasa bado vinaitekeleza vikiwa na dhana ya utengano.
No comments:
Post a Comment