Mgomo wa mabasi kizungumkuti - LEKULE

Breaking

29 Apr 2015

Mgomo wa mabasi kizungumkuti


Dar es Salaam. Hali ya sintofahamu imetawala mpango wa wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani kufanya mgomo wa wiki moja kuanzia leo, kutokana na baadhi kutokatisha tiketi za safari za leo na wengine kukatisha.

Zaidi ya mabasi 300 hufanya safari kila siku kati ya Dar es Salaam na mikoa mingine pamoja na nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Burundi la Rwanda.

Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) kilitangaza juzi kufanya mgomo huo kuanzia leo kupinga uamuzi wa Serikali kushusha nauli kwa hoja ya kuendana na kuporomoka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, wakisema kuwa nishati hiyo ni sehemu ndogo ya gharama za biashara ya huduma za usafiri.

Uamuzi wa kushusha nauli ulitangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) wiki mbili zilizopita na utekelezaji wake unatakiwa uanze Mei Mosi.

Kutokana na hali hiyo, Taboa iliwataka mawakala wake kutokatisha tiketi kuanzia jana kwa abiria wanaotaka kusafiri kuanzia leo hadi hapo Sumatra itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli ya zamani kuendelea kutumika kwa maelezo kuwa gharama za uendeshaji ziko juu tofauti na faida zinazoletwa na kushuka kwa bei ya mafuta pekee.

Pamoja na kauli hiyo, jana baadhi ya kampuni ziliendelea kukatisha tiketi kwa ajili ya abiria kusafiri leo, jambo ambalo katibu wa Taboa, Enea Mrutu alilielezea kuwa ni usanii kwa kuwa leo hakuna basi litakaloondoka kituoni.

“Tulishakubaliana katika kikao cha jana (juzi) kuwa mgomo wa wiki moja utaanza kesho (leo), hivyo kuanzia leo hakuna tiketi itakayouzwa. Kama kuna wanaoouza wanafanya sanaa tu kwani hakutakuwa na safari yoyote kesho (leo),” alisema.

Mgomo huu wa Taboa unakuja ikiwa ni wiki tatu tangu madereva walipogoma kwa takriban saa tisa na kusababisha kero kubwa kwa wasafiri kwenye mikoa mingi na kusababisha Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka kutangaza kusitishwa kwa kanuni mpya za kudhibiti usajili wa madereva na udhibiti wa safari.

Mawakala wachanganywa

Tangu alfajiri ukataji tiketi ulikuwa unafanywa kama kawaida katika ofisi zote, zaidi ya 40 zilizopo katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) huku kukiwa na uhakika wa safari leo.

Hali ilibadilika kuanzia saa 6:00 mchana baada ya taarifa za kukanganya kuzagaa katika ofisi hizo, huku baadhi ya mawakala na makarani wakipokea maagizo kutoka kwa wamiliki wa mabasi husika kusitisha kazi hiyo.

Katika ofisi namba 14, gazeti hili lilishuhudia zaidi ya abiria sita waliokuwa wanataka tiketi za kwenda Iringa wakiambiwa kuwa hakuna uhakika wa usafiri hivyo warudi leo ili kujiridhisha kabla hawajaondoka.

“Siwezi kuuza tiketi kwa sababu sina uhakika na safari kesho (leo). Sitaki kupokea nauli za watu halafu kesho wakaanza kunipa malalamiko pindi watakapoona gari haliondoki,” alisema Agness Nyagabona baada ya kukataa kuuza tiketi kwa mmoja wa abiria aliyeletwa ofisini hapo.

Mabasi ya kampuni ya Nyagawa Safari yanayofanya safari zake kwenda Iringa hayakuuza tiketi tangu asubuhi kwa maelekezo kutoka kwa wakala wa kampuni hiyo ambaye aliagizwa na mmiliki wake.

Emmanuel Mwanyika, karani wa mabasi hayo, alisema kuwa walipewa maagizo na wakala wao kutouza tiketi kwa siku hiyo mpaka watakapoelekezwa vinginevyo.

Wengine ambao walisitisha uuzaji wa tiketi kwa jana ni pamoja na Super Feo, Al-Saedy, Takbir na Wibonela Express. Wengi walieleza kuwa kuna uwezekano wa mabasi yao kupigwa mawe endapo watakaidi kutii mgomo huo.

Saa 6:00 mchana, ofisi ya Super Feo ilipokea taarifa ya kusitisha uuzaji wa tiketi na kwamba taarifa itolewe mapema kwa wasafiri waliokuwa wamekata tiketi. Iliagizwa kuwa watakaotaka warudishiwe nauli au wabadili tarehe ya safari.

Zipo baadhi ya ofisi ambazo ziliendelea kuuza tiketi kama kawaida huku zikieleza kuwa hazikupewa taarifa na wamiliki wa mabasi husika, hivyo kutofuata mkumbo wa wenye taarifa au wasiwasi wa mgomo.

Kwenye ofisi za kampuni za Karaghan, Prince Shabaha, Shabiby, Machinga High Class, ABC Upper Class, Dar Express na Abood kazi ya ukatishaji tiketi ilikuwa ikiendelea kama kawaida.

Saumu Maftali wa Shabiby alisema: “Nasikia kuwa kulikuwa na mkutano wa wamiliki ambao ulipitisha mgomo huu. Lakini mpaka sasa hatujapewa maelekezo yoyote hivyo tunaendelea kama kawaida. Kama kutakuwa na mabadilikom basi tutaambiwa cha kufanya,” alisema Saumu.

Sumatra CCC

Baraza la Ushauri la watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra CCC) lilisema kuwa mgomo huo haujafuata taratibu kwamba endapo utatekelezwa utakuwa unavunja sheria.

No comments: