Mambo Makubwa Matatu Yanayompa Kichwa Mh. Sitta Kugombea kiti Cha Urais Mwaka Huu - LEKULE

Breaking

20 Apr 2015

Mambo Makubwa Matatu Yanayompa Kichwa Mh. Sitta Kugombea kiti Cha Urais Mwaka Huu


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema anasubiri kukamilika kwa utaratibu wa CCM wa kugombea urais ili aingie rasmi kwenye mbio hizo kwa kuwa anaridhika na mambo matatu ambayo anasema yanamfanya ashawishike kugombea nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini.

Sitta, mwanasiasa mkongwe na Spika wa Bunge la Tisa, ni mmoja kati ya makada wa chama hicho tawala wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais kumrithi Jakaya Kikwete, ambaye anamaliza vipindi vyake viwili vya urais Oktoba mwaka huu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Sitta alisema zaidi ya mambo hayo matatu, anaamini ana ushawishi mkubwa na Watanzania wengi wanamwamini katika utendaji kazi wake.

“Nina mengi nimefanya kutokana na historia yangu ya kiutendaji na ndiyo nitakayoitumia kama mtaji utakaonibeba kwenye harakati hizi,” alisema.

Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alitaja mambo hayo matatu ambayo ni mtaji wake kuwa ni 1.Uendeshaji wake wa chombo hicho cha kuandika Katiba, 2.Uendeshaji wake wa Bunge na
3.Uzoefu wake wa muda mrefu kwenye nafasi mbalimbali alizowahi kushika.

“Niliendesha Bunge la Katiba kwa mafanikio na hata kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa,” alisema Sitta.

“Watanzania wataangalia wenyewe historia yangu kwani mimi ndiye mwenyekiti niliyefanikisha kutimiza ndoto za Watanzania kupata Katiba mpya kupitia Bunge Maalumu la Katiba, haikuwa rahisi katika tukio hilo,” alisema.

Hata hivyo, Bunge la Katiba halikuisha kwa maridhiano baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kususia vikao kwa madai kuwa chombo hicho kiliweka pembeni Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi.

Juhudi za Sitta kuwarejesha vikaoni ziligonga mwamba, lakini mchakato ukaendelea hadi Katiba Inayopendekezwa ilipopatikana.

Sitta alisema mtaji wake mwingine katika mbio za urais ni na kuimarisha demokrasia ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Mimi ndiye niliyebadilisha Bunge baada ya kubadilisha kanuni za Bunge mwaka 2007, ambazo zilitoa uhuru, haki na usawa kwa wabunge wote bila kujali wapinzani,” alijigamba.

No comments: