Mama Ajifungua Mtoto na Kisha Kumtupa Katika Shimo la Takataka ( Jalala) jijini Mwanza - LEKULE

Breaking

14 Apr 2015

Mama Ajifungua Mtoto na Kisha Kumtupa Katika Shimo la Takataka ( Jalala) jijini Mwanza



Mama mmoja mkazi wa kata ya Mkuyuni-Sokoni wilayani Nyamagana jijini Mwanza (jina lake halikufahamika mara moja) amejifungua mtoto wa kiume na kisha kumtupa kwenye shimo la kutupa taka (jalala) eneo a Mkuyuni jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa watoa taarifa kwa viongozi wa serikali aliyetoa sharti la kutotajwa jina lake amesema:

“Mimi ni mfanya usafi hapa Mkuyuni, wakati ninaenda kumwaga uchafu pale dampo nikakuta kitoto kichanga kimetupwa maeneo hayo ndipo nilipoenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkuyuni-Sokoni ili wafanye utaratibu wa kukitoa hapo:”

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mkuyuni, Godwin Peter Kyangara, amesema: “Mimi nimeletewa hizi taarifa za mtoto huyu aliyetupwa maeneo haya mida ya saa 2:30 asubuhi, baada ya kupokea taarifa hizo ikabidi nikatoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ndipo walipokuja kuuchukua mwili wa mtoto huyo.”

Inasemekana kwamba mtoto huyo alikuwa tayari ana umri wa miezi tisa hivyo mzazi wake alikuwa tayari amejifungua ndipo alipoamua kumtelekeza kwenye shimo hilo la kutupa takataka.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Mkuyuni, Charles Fashion, ameeleza kuwa ameshangazwa na kitendo hicho cha mwanamke kujifungua mtoto na kumtupa jalalani ambapo alisema inabidi atafutwe na apewe adhabu iwe fundisho kwa akina mama wengine wenye tabia kama hizo katika jamii.

Aidha, Jeshi la Polisi jijini Mwanza limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa bado juhudi za kumtafuta mwanamke huyo aliyetenda unyama huo zinaendelea ili afikishwe mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

No comments: