Malasusa: Waumini Wengi ni Washirikina - LEKULE

Breaking

6 Apr 2015

Malasusa: Waumini Wengi ni Washirikina



Matukio ya ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi, vikongwe na watu wa makundi mengine ya kijamii nchini, yametajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hofu na kutojiamini kwa baadhi ya watu, hivyo kujikuta wakitumia nguvu za ziada kutaka kufanikisha mambo yao, badala ya kumtegemea Mungu.

Hayo yamebainishwa kwenye Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front na Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk Alex Malasusa.

Alisema hofu na kukosa uhakika ni chanzo kikubwa cha dhambi jambo ambalo linawafanya watu kuingia katika matendo ya ushirikina na mauaji ya binadamu wenzao.

“Watu wengi wamekuwa wakishiriki ushirikina na si kwamba wanapenda ushirikina, hawapendi, lakini wamejawa na hofu na hawana uhakika na ndio chanzo cha dhambi. Kumekuwapo na matukio mengi ya ushirikina ambayo si kawaida kwa binadamu aliyeumbwa na akili akayatenda."

Malasusa aliongeza: “Haijalishi umesoma kiasi gani, leo hii imethibitika wasomi wengi wameingia kwenye ushirikina, haijalishi una hali gani ya kiuchumi, wafanyabiashara wengi wamejiingiza kwenye ushirikina, haijalishi unapenda ibada kiasi gani, imethibitika tunaoingia na kutoka ibadani bado tunashiriki ushirikina.

“Ndio maana tunasikia matendo ya kusikitisha ya binadamu kwenda kuua binadamu wenzao kama albino, vikongwe kutokana na kujawa na hofu, eti wanaamini kwa kuua albino watapata fedha au mafanikio kwenye uchaguzi, huo ni uovu na akili za kishetani. Yesu aliyefufuka ndio atakayekupa mafanikio.”

No comments: