Mahakama Yaamuru Mtuhumiwa wa Escrow Akamatwe - LEKULE

Breaking

2 Apr 2015

Mahakama Yaamuru Mtuhumiwa wa Escrow Akamatwe



Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma anayekabiliwa na kesi ya kupokea Sh milioni 323.4, kwa kuwa hajafika mahakamani.

Aidha imetoa hati kwa wadhamini wa Mujunangoma kufika mahakamani kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua kutokana na kitendo chao na mshitakiwa kutofika mahakamani.

Hakimu Mkazi Emmilius Mchauru alitoa hati hizo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kusikiliza pingamizi, lililowasilishwa na upande wa utetezi.

Awali, Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai aliiomba mahakama kutoa hati hizo kwa kuwa mshitakiwa na wadhamini wake hawajafika mahakamani bila kutoa taarifa.

Hakimu alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa tena. Mujunangoma anadaiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 323.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana nje ya mahakama kutoka kwa watu wanaodai ni ndugu wa mshitakiwa, Mujunangoma alipata shinikizo la damu akiwa njiani kuja mahakamani hivyo alipelekwa katika Hospitali ya Arafa, Tabata, na kulazwa.

Ilidaiwa kuwa walitoa taarifa kwa mdhamini ili afike mahakamani kutoa taarifa lakini alichelewa na kukuta kesi imeshatajwa na hati hizo zimetolewa.

Mujunangoma anadaiwa Februari 5, 2014 katika Jengo la Benki ya Mkombozi, alipokea rushwa ya Sh milioni 323.4 kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya kufua Umeme ya VIP Engineering and Marketing ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Inadaiwa Mujunangoma, alipokea fedha hizo kupitia akaunti 00120102602001 kama tuzo baada ya kushughulikia masuala ya Kampuni ya IPTL kama mfilisi, bila kumtaarifu mkuu wake wa kazi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

No comments: