Kenya yafuta leseni za wakala wa riadha - LEKULE

Breaking

14 Apr 2015

Kenya yafuta leseni za wakala wa riadha


Rais wa chama cha wanariadha wa kulipwa cha Kenya Wilson Kipsang amepinga vikali mpango wa chama cha riadha cha Kenya kuwasimamia wanariadha ambao meneja wao wamesimamishwa kwa muda wa miezi sita na chama hicho.

Mwenyekiti wa chama cha riadha cha Kenya Isaiah Kiplagat ametangaza Federico Rosa wa Italia na Gerald Vandeveen wa Uholanzi wamefungiwa kwa miezi sita wakishukiwa kuhusika na dawa za kuongeza nguvu.

Kiplagat anasema watafanya uchunguzi kwa miezi hiyo sita na endapo watapatikana na hatia watafungiwa.

Uamuzi huo unatokana na kashfa ya wanariadha wa Kenya kutumia dawa za kuongeza nguvu.

Kufikia sasa zaidi ya wanariadha 30 wa Kenya wamepatikana na hatia ya kutumia dawa hizi za kusisimua misuli akiwemo bingwa mara mbili wa Boston Marathon Rita Jeptoo ambaye amefungiwa mwa miaka miwili.

Kiplagat ameeleza kwa kipindi cha miezi hiyo sita ni chama hicho kitawakilisha wanariadha kama maajenti wao.

Lakini Kipsang ambaye pia ni bingwa wa Boston Marathon anasema hawatakubali kamwe kusimamiwa na chama hicho kwa sababu hawana imani nao kwa maswala ya fedha.

Kipsang amesema ni makosa kwa chama cha riadha nchini Kenya kufungia maneja wao bila kuwajulisha na kuwa na ushahidi wanahusika na madawa ya kuongeza nguvu.

Ameawambia wazi wakuu wa chama hicho uamuzi huo wa kuwasimamia ni ndoto kubwa kwa sababu haitawezekana, huku kukiwa na madai ya ufujaji wa pesa dhidi yao.

Anasema watazungumza na wizara ya michezo isajili maajenti wengine ili nao wajiunge nao kwa muda huo meneja hao wawili watakua wamesimamishwa.

Ni wazi kwamba maneja hao nao watajitetea kwa adhabu hiyo na huenda wakachukua hatua za kisheria.

Miongoni mwa wanariadha ambao Rosa anawakilisha ni bingwa wa dunia mbio za mita mia nane Eunice Sum, Asbel Kiprop na Vivian Cheruiyiot,

naye Vandaveen baadhi ya wakimbiaji anaowakilisha Kipsang na anayeshikilia rekodi ya dunia ya marathon Dennis Kimetto.

No comments: