Karaha za kupanga nyumba Dar - LEKULE

Breaking

8 Apr 2015

Karaha za kupanga nyumba Dar



Dar es Salaam. Karibu nusu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaishi katika nyumba za kupanga ambazo pamoja na kuwa ni chanzo cha mapato kwa wanaozimiliki, kwa upande mwingine ni karaha kwa wapangaji.

Utafiti uliofanywa kwa wapangaji pamoja na madalali katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam umebaini kadhia wanazokabiliana nazo zikiwamo masharti makali na mikataba bubu ya upangaji.

Miongoni mwa kadhia hizo ni pamoja na kufukuzwa kwenye nyumba kabla ya mkataba kwisha, kupewa masharti magumu kama vile kukataa wapangaji wenye watoto, kupika aina fulani ya chakula na wamiliki wengine wakichagua wapangaji kutokana na dini zao au makabila.

Matatizo mengine ni foleni za kwenda chooni ambacho pia ni bafu, ratiba za usafi, matatizo ya maji na nyumba kutokufikika kirahisi. Katika maeneo ya Tandale, Kinondoni na Vingunguti ilibainika kuwa wenye nyumba ni wepesi kuwageuka wapangaji hata kama waliandikishiana mkataba.

“Unaweza kukubaliana na mwenye nyumba ukaingia naye mkataba vizuri, lakini baada ya siku chache, anakwambia uondoke wakati ulishampa kodi, anaweza kukutafutia sababu yoyote tu,” alisema dalali wa Tandale hadi Kinondoni Studio, Nassoro Maskani.

Dalali mwingine, Saleh Mkumbila alisema kuna nyumba ambazo wanataka wapangaji wa kike tu kwa sababu wapangaji wa kiume wanaweza kuwarubuni mabinti wa wenye nyumba. Mkazi wa Magomeni kwa Bibi Nyau, Selemani Kaisi (maarufu Cholo), alisema ni kawaida kukutana na masharti mazito ya kutatanisha kutoka kwa wenye nyumba.

“Si ajabu kumsikia mwenye nyumba akiwa hataki wapangaji wanaume au wanawake. Kila mmoja ana sababu zake,” alisema.

Mkazi wa Barafu, Kigogo Mburahati, Anna Yohana alisema wapo wenye nyumba ambao wanataka wapangaji wanaume ambao hawajaoa na wanafanya kazi. “Hawa wana faida kwa sababu hawana usumbufu lakini hawafanyi usafi, badala yake wanatakiwa kutoa fedha ya usafi wa choo na uwanja,” alisema Yohana.

Ujanja wa madalali

Katika biashara ya kupanga nyumba na kupangisha, kundi la madalali linatajwa kuongoza kwa utapeli. Dalali mmoja anaweza kuwapeleka watu 10 katika chumba kimoja kwa siku moja, kila mtu kwa muda wake na kila mmoja anampa Sh5,000 ya udalali, kwa siku atakusanya Sh50,000. “Yaani madalali ni wababaishaji sana na ndiyo wanaosababisha nyumba zipande bei Sinza kwani anaweza akakutajia mazingira ya chumba ukahisi ni kizuri sana lakini ukifika unakuta tofauti,” alisema mkazi wa Sinza, Ruth Ahazi na kuongeza kuwa lengo la dalali ni kutaka mgawo wake, kodi ya mwezi mmoja, uwe mkubwa. Mmoja wa madalali kutoka Sinza, Chesco Athanas alisema huwa wanawatoza wateja fedha ya kuwapeleka kuangalia vyumba kufidia usumbufu na muda wao. Hata hivyo, alisema yapo baadhi ya maeneo kama Buza Barabarani, Pile, Temeke Mwisho, Mwembe Yanga ambako kuna nyumba nzuri lakini kodi zake ni kubwa kutokana na kuwa na kuwa salama zaidi ikilinganishwa na sehemu nyingine. “Huko ipo nyumba ya Sh200, 000 kwa mwezi lakini gari, pikipiki unalaza kwenye kituo cha mafuta kilichopo jirani au kwenye ofisi za chama, hizi zipo nyingi wateja wake hawapatikani sana,” alisema dalali kutoka Tandika Yusuf Mkumba. Katika maeneo mengi ambayo Mwananchi iliyatembelea wenye nyumba waliweka masharti ya mpangaji kuwahi kurudi, kukataa ulevi kupita kiasi na masharti kwa vijana ambao hawajaoa. “Vijana ambao hawajaoa wanakatazwa kuingiza wanawake tofauti, hili wenye nyumba wanalipigia kelele sana,” alisema Cholo. Huko Sinza, madalali wanayataja masharti mbalimbali wanayopata wapangaji wa maeneo hayo kuwa ni kama vile kutochoma ubani. Wamiliki wa nyumba hasa wa dini ya Kikristo wengi kwao hili ni tatizo kidogo na kwa wenye nyumba wenye msimamo mkali wa dini ya Kiislamu wengi wanakataza familia kubwa na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Mwenye nyumba atetea

Mmiliki wa nyumba iliyoko Tabata, Mawenzi, Kashushu Kisala alisema masharti kwa mpangaji ni muhimu wakati wa kuingia mkataba kwani bila masharti, nyumba haitadumu, haitakuwa na heshima wala kodi haitapatikana kwa wakati. “Masharti mengine ni kwa manufaa ya jamii nzima, kama ulevi, wanawake wengi au kuchelewa kurudi. Huwezi kunisumbua kwenye nyumba yangu,” alisema Kisala. Matatizo ya nyumba na upangaji yaliwahi kufikishwa bungeni, hasa kwa kipengele cha mpangaji kutakiwa kulipa kodi ya mwaka au miezi sita kwa mkupuo wakati mapato yake, hasa mshahara, yanapatikana kwa mwezi.

Februari 12, 2012, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba aliomba kupeleka muswada wa Sheria ya Kudhibiti Upangaji wa Nyumba za Makazi. Katika muswada huo, January ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alitaka sheria hiyo iweke utaratibu na udhibiti wa sekta ya upangaji wa nyumba nchini kwa ujumla. Kadhalika, alitaka sheria hiyo iwezeshe kuanzishwa kwa mamlaka ya usimamizi wa sekta ya nyumba, real estate regulatory authority (Rera). “Sheria hiyo itaainisha wazi haki na wajibu wa wapangaji na wenye nyumba, pia itasaidia wapangaji na wenye nyumba kupata haki zao,” alisema January. Hata hivyo, hoja yake binafsi ilipingwa na Serikali na kukataliwa na Bunge. Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema pamoja na kuwa hoja hiyo ni ya msingi, Serikali inahitaji muda kwanza kumaliza sera ya nyumba ili vyombo stahiki vifanye kazi yake kwa kuangalia sheria gani na uhakiki utakaowekwa ili suala hilo lishughulikiwe kwa haraka.

No comments: