Wakati Taifa likiadhimisha kumbukumbu ya miaka 43 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh
Zanzibar. Wakati Taifa likiadhimisha kumbukumbu ya miaka 43 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, wananchi wa Zanzibar wamesema awamu saba za viongozi waliomfuatia wameshindwa kufikia hata nusu ya maendeleo aliyoyafanya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi walisema maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wa hayati Karume aliyeuawa mwaka 1972 ni makubwa ikiwemo kuanzisha sera ya makazi na kuwajengea nyumba za kisasa wananchi wake.
Pia ujenzi wa viwanda, kutekeleza kwa vitendo sera ya elimu bila malipo na huduma za maji na afya kutolewa bure.
Mkazi wa Michezani, Said Ali Mohamed alisema Karume alianzisha vituo vya kuwahifadhi wazee wasiojiweza na yatima kwa kuwajengea nyumba za kisasa na kuwapatia huduma muhimu ikiwa ni utekelezaji wa sera ya maisha bora kwa kila mwananchi wake.
Alisema hayati Karume alijenga barabara za kisasa za njia mbili na kuwa nchi ya kwanza kuwa na barabara za haina hiyo Afrika Mashariki na Kati na alianzisha kituo cha televisheni ya rangi na kuwa ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mkazi wa Mkunazini, Suleimani Ali ‘Sukari’ alisema malengo ya Mzee Karume yametupwa ndiyo maana viwanda vyote vimekufa kutokana na kukosekana kwa mipango mizuri ya uchumi.
Alisema Zanzibar ilikuwa na kiwanda cha kutengeneza viatu, maziwa, magodoro, mafuta ya kupikia, soda, sigara, masufuria, nguo pamoja na viwanda vidogovidogo lakini sasa vimebakia historia na kusababisha ongezeko kubwa la vijana wasiokuwa na kazi.
“Kama mambo aliyokuwa ameyapanga yangelikuwa yakifuatwa na viongozi waliomfuatia, nchi ingebadilika na kujenga uchumi imara,” alisema Suleiman.
Alisema Karume alipiga vita rushwa kwa vitendo na kusimamia haki za wananchi wake bila ya kujali rangi kabila na kuwaunganisha Wazanzibari baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Mkazi wa Mbweni, Juma Makame Mcha alisema: “Karume aliwapenda wananchi wake na mambo aliyoyafanya katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wake hakuna kiongozi hata mmoja aliyefikia hata nusu yake.”
Mkazi wa Jang’ombe, Mwajuma Juma Suleiman alisema, Karume alifanya mambo mazuri kwa wakati mdogo kwa sababu mali ya wananchi ilitumika kuwaletea maendeleo badala ya kujinufaisha na familia yake.
Alisema Zanzibar ingepiga hatua kama sera za marehemu Karume zingesimamiwa kwa nguvu... “Karume alipenda nchi na wananchi wake, kila jambo zuri anawasogezea wananchi wake, leo wananchi waliopewa ardhi na Karume sasa wananyang’anywa na baadhi ya vigogo katika Serikali.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema awamu zote zimefanya mambo makubwa ya maendeleo kulingana na hali ya uwezo wa kiuchumi pamoja na ongezeko la idadi ya watu.
Alisema kushuka kwa uzalishaji wa zao la karafuu kutoka tani 24,000 hadi 3,000 pamoja na kuanguka kwa bei ya zao hilo miaka ya 1980 kutoka dola 9,000 kwa tani hadi 600 katika soko la dunia, kuliathiri upatikanaji wa mapato ya Serikali na huduma nyingi za jamii.
“Sababu kubwa ya kufa viwanda vyetu ilitokana na kukosekana kwa malighafi, masoko na utaalamu lakini Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kukaribisha uwekezaji katika sekta ya viwanda na tayari wafanyabiashara wakubwa wameanza kujitokeza kuendelea sekta hiyo.”
Kuhusu chuki za kisiasa, Waziri Aboud alisema mabadiliko ya mfumo wa kisiasa kutoka chama kimoja na kuingia vyama vingi yamechagia na kuwataka wananchi kufanya siasa za kistaarabu na kuweka mbele uvumilivu wa kisiasa.
Hitima ya marehemu Karume inafanyika leo Makao Makuu ya CCM na inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais Dk Mohamed Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.
No comments:
Post a Comment