Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM na kwamba ile yenye upinzani itaandikishwa kwa kulipua ili watu wengi wenye sifa ya kupiga kura wasiandikishwe.
NEC ilianza kuboresha Daftari la Wapigakura kwa kuandikisha wananchi wa Mkoa wa Njombe, ambako watu 300,080 waliandikishwa kati ya 392,634 waliotarajiwa na sasa inaelekea mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa baada ya kupokea mashine nyingine 1,600. Kazi hiyo itaendelea kwenye mikoa ya Katavi, Mbeya na Dodoma wakati mashine 1,600 zaidi zitakapowasili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amesema hilo ni jambo jipya kwake kwa kuwa hawakuangalia suala hilo wakati wa kupanga mikoa hiyo.
Akizungumza jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini akitokea Marekani, Dk Slaa alisema wamegundua kwamba mwishoni mwa kazi ya uandikishaji kwenye mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, watu wengi hawataandikishwa.
“Tumegundua hujuma zao, NEC wameanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM. Huko wanajitahidi kuandikisha wapigakura wote na wanachukua muda mrefu,” alisema Dk Slaa akionekana kurejea Mkoa wa Njombe ambako NEC imetumia takriban miezi miwili kuandikisha wapigakura.
“Mikoa yenye ngome ya Chadema na vyama vingine vya upinzani itakuwa ya mwisho kuandikisha wapigakura na uandikishaji huo utakuwa wa harakaharaka ambao utawaacha mamia ya watu bila kuandikishwa kwa sababu muda utakuwa hautoshi,” alisema Dk Slaa.
Alisema suala hilo linaweza kuvuruga uchaguzi, hasa ikizingatiwa kwamba mchakato wa uandikishaji umekuwa na sintofahamu nyingi.
Kwa mujibu wa matokeo ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, CCM ilivuna kura 128,809 katika majimbo matatu ya mkoani Njombe (Njombe, Ludewa na Makete) wakati huo ukiwa ndani ya Mkoa wa Iringa. Chadema ilifuatia kwa kupata kura 36,928 na CUF/NCCR zilipata kura 1,670
Kwa kujumuisha kura hizo na majimbo mengine ya Iringa CCM ilipata jumla ya kura 299,799 ikifuatiwa na Chadema iliyopata kura 76,010. CUF na NCCR-Mageuzi zilipata jumla ya kura 3,137. Hadi sasa upinzani una mbunge mmoja tu kwenye mikoa hiyo miwili, Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.
Kwenye uchaguzi wa Rais mwaka 2010 mkoani Lindi, mgombea wa CCM alipata kura 150,118 akiwa mbele ya mgombea wa CUF aliyepata kura 64,875 wakati wagombea wa Chadema na NCCR walipata jumla ya kura 12,880.
Wapinzani wana wabunge wawili mkoani Lindi ambao ni Selemani Bungera wa Kilwa Kusini na Salum Barwany wa Lindi Mjini, wote kutoka CUF.
Mkoani Mtwara, mgombea urais wa CCM alipata kura 213,844 akimuacha mbali mgombea wa CUF aliyepata kura 81,953, huku wagombea wa Chadema na NCCR wakipata jumla ya kura 82,233. Hakuna mbunge kutoka upinzani mkoani Mtwara.
Takwimu za 2010 pia zinaonyesha kuwa mkoani Ruvuma, mgombea urais wa CCM alipata kura 198,090, akimuacha kwa mbali mgombea wa Chadema aliyepata kura 36,044, CUF (28,873) na NCCR kura 397.
“Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete atuepushe na vurugu zinazoweza kutokea. Kwa kuwa anamaliza muda wake Oktoba 28, mwaka huu, ahakikishe kwamba NEC inaandikisha watu wote bila kupendelea mikoa yenye ngome ya CCM,” alisema.
Alisema Rais anatakiwa ahakikishe kwamba kwa kutumia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/16, NEC inawezeshwa kupata fedha za kutosha ili iweze kuandikisha watu kwa ufanisi zaidi.
“Tungependa Rais Kikwete aiache nchi ikiwa salama kwa sababu kasoro zilizojitokeza katika zoezi hili ni nyingi na zikiendelea zinaweza kuvuruga uchaguzi... uchaguzi ndiyo kipaumbele chetu mwaka huu, ” alisema.
Alisema Serikali ihakikishe inashinikiza kuingizwa kwa vifaa vya BVR ambavyo vinaingia kwa mafungu ili wananchi wenye sifa waweze kuandikishwa.
Hadi sasa kati ya mashine za BVR 8,000 ambazo zinatakiwa kuingizwa nchini kwa ajili ya kazi hiyo, ni 2,098 tu ndizo ambazo zimeshawasili.
NEC yajibu
Akijibu madai hayo Jaji Lubuva alisema hilo ni jambo jipya kwake: “Hatufahamu kwamba mikoa hiyo ni ngome ya CCM,” alijitetea Jaji Lubuva.
“Tumeanza kuandikisha bila kujali kwamba hiyo ni ngome ya chama fulani cha siasa.” Alisema Dk Slaa anachotakiwa kufahamu ni kwamba kila mwananchi mwenye sifa atakayejitokeza kuandikishwa, ataandikishwa.
“Sisi hatuangalii ngome za vyama vya siasa, kazi yetu ni kuandikisha bila kujali hapa ni ngome ya nani,” alisema.
Ziara ya Marekani
Dk Slaa, ambaye aliambatana na mkewe, Josephine Mushumbushi alisema wamekubaliana kuanzisha ushirikiano hasa katika nyanja za kiuchumi na Jimbo la Indiana.
“Tumekubaliana kwamba tukiingia Ikulu tutapenda kuwa na wawekezaji, lakini tofauti na ilivyo sasa. Watakaotaka kuja kuwekeza nchini watatakiwa kufanya hivyo kwa kufuata masharti yetu na siyo masharti yao,” alisema.
Dk Slaa aliwasili jana saa 2.30 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Qatar Airways na kulakiwa na wafuasi wa chama hicho waliokuwa na bango linalosomeka, “Karibu nyumbani rais wa awamu ya tano Dk Willibrod Slaa.”
Dk Slaa alikwenda Marekani kwa mwaliko wa Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence pamoja na taasisi mbalimbali, vikiwamo vyuo vikuu, baada ya kutambua mchango wake na wa chama chake katika masuala ya kisiasa na kijamii katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Akifafanua, alisema alipata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za vyuo na kujionea namna nchi hiyo inavyothamini tafiti za wasomi. “Wenzetu wamewekeza kwenye tafiti, moja ya vipaumbele vikubwa kwa Serikali yao ni kutoa fedha za kutosha kwenye tafiti tofauti na hapa nchini ambako utafiti siyo kipaumbele chetu,” alisema.
Alisema pia alitembelea shamba la mifugo lenye ng’ombe wa maziwa 15,000 ambako alikuta ng’ombe mmoja anatoa lita 27 kwa siku na kwamba linatoa mchango mkubwa katika uchumi.
“Nikajiuliza, sisi Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi Afrika, lakini wanasaidia vipi katika uchumi wetu wakati hata viatu tunaagiza kutoka China wakati tuna ngozi ya kutosha?” alisema.
Mauaji ya Afrika Kusini
Dk Slaa pia amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuacha kufanya siasa wakati maisha ya Watanzania wanaoishi Afrika Kusini, yako hatarini.
“Watanzania hao wanatakiwa kurudishwa nchini haraka hadi hali ya usalama itakaporejea Afrika Kusini. Serikali isikwepe jukumu la kuwarudisha wananchi wake,” alisema.
Alisema anashangazwa na kauli ya Membe kwamba Mtanzania aliyekufa Afrika Kusini aliuawa kwa ujambazi.
“Unadhani watasema ameuawa kwa sababu gani wakati hata polisi wa Afrika Kusini wako upande wa vijana hao wanaofanya vurugu? Alitakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha kwamba Mtanzania huyo aliuawa kwa ujambazi,” alisema.
Juzi, Membe alikaririwa akisema kuna Watanzania watatu ambao wamekufa lakini akakanusha kuwa waliuawa kwenye vurugu zinazoendelea Afrika Kusini. Miongoni mwa waliokufa ni Rashid Jumanne ambaye aliuawa kilomita 90 kutoka mji wa Durban.
ACT- Wazalendo
Akizungumzia ujio wa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), alisema kwa kifupi: “Nakiona kama vyama vingine lakini siyo tishio kwa Chadema kwani chama chetu kina misingi imara ambayo inakifanya kila siku kuwa juu,” alisema kwa kifupi
No comments:
Post a Comment