MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge juzi aliokolewa kwa risasi katika vurugu za kundi la wananchi, waliomvamia karibu na ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Simiyu na kusababisha taharuki katika ofisi za chama hicho.
Mmoja wa watu waliokuwa kwenye gari la mbunge huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa na msafara wake kutekeleza shughuli za ubunge jimboni mwake, ndiye aliyefyatua risasi hewani ili kutawanya umati huo.
Hata hivyo, hali hiyo ilitafsiriwa na Chadema kuwa ni mkakati wa mbunge huyo wa kuwafanyia fujo katika ofisi zao, hivyo kulifikisha suala hilo Polisi ambako wamefungua jalada.
Madai ya tukio hilo yaliyotolewa na John Heche, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), yamethibitishwa Jeshi la Polisi ambalo limesema aliyefyatua risasi si Chenge, bali mmoja wa watu waliokuwa kwenye gari lake.
Risasi Chadema
Akizungumza jana, Heche alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1:30 jioni katika ofisi za chama hicho mkoa wa Simiyu zilizoko eneo la Salunda.
“Mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa chama hicho uliohutubiwa na Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, John Mnyika baadhi ya wanachama walipanda magari na wengine kutembea kwa miguu ili kwenda kwenye ofisi zao za mkoa ambako watu walishtuka kumuona mbunge huyo akishuka katika gari lake,” alianza kuelezea Heche.
Aliongeza kuwa, wakati wakiendelea na kikao, magari mengine matano yanayodaiwa kuwa ya msafara wa Chenge yalifika eneo la ofisi ya Chadema na kusimama na huku gari moja la matangazo likipiga muziki wa `CCM’ kwa sauti kubwa, huku mbunge huyo akidaiwa alishuka na kuanza kucheza.
“Kutokana na kitendo hicho, mmoja wa walinzi wa Chadema aliwaomba waondoke eneo hilo na pia waache kupiga muziki huo kwani kuna kikao cha ndani cha viongozi wa chama hicho kinachoendelea lakini waligoma.
“Mara lilifika kundi la wapenzi na wanachama wa Chadema na kuyazunguka magari hayo na Chenge kuingia ndani ya gari ndipo risasi zilipopigwa kutoka katika gari alilokuwemo Chenge ili kutawanya kundi hilo ambalo nalo lilianza kuwashambulia kwa mawe na hivyo kusababisha taharuki na kusababisha mkutano huo kuvunjika,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa Chadema mkoa wa Simiyu waliripoti tukio hilo Makao Makuu ya Polisi wilaya ya Bariadi na kutoa malalamiko yao juu ya tukio hilo na kufunguliwa faili namba BAR/ RB/1195/2015.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema kuwa aliyefyatua risasi si Chenge, bali ni kijana Ahmed Ismail aliyekuwa katika gari la Mbunge huyo, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na Waziri aliyeziongoza wizara kadhaa, zikiwemo Katiba na Sheria na Miundombinu.
Kwa mujibu wa Kamanda Mushi, Chenge alikuwa akitoka katika mkutano wa CCM akienda nyumbani kwake kupitia Barabara Kuu moja iliyopo katika jimbo hilo.
Alifafanua kuwa wakati akienda nyumbani kwake, alikutana na watu waliozuia gari lake barabarani, ambapo Chenge alitoka na kuzungumza nao huku wao wakimshangilia.
Kamanda Mushi alidai kuwa wakati Chenge akizungumza na wananchi hao, kulitokea watu wengine kutoka ilipo ofisi ya Chadema ambayo haikuwa mbali na eneo hilo, ambao walianza kurushia mawe msafara wa mbunge huyo na kumlazimisha kuingia ndani ya gari lake.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Mushi alidai kuwa Ahmed aliyekuwa ndani ya gari la Chenge, alilazimika kupiga risasi tatu angani ili kutawanya wananchi waliomsimamisha Chenge na kutoa nafasi ya mbunge huyo kupita.
Alipotakiwa kueleza hatua zilizochukuliwa, Kamanda Mushi alisema alichokifanya Ahmed si makosa kwa kuwa ndivyo watu wanaomiliki silaha, walivyoelekezwa kwamba kunapotokea hatari wapige risasi angani kwa ajili ya kutoa onyo.
Alieleza kuwa silaha hiyo, ingawa imechukuliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi, lakini ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed. Alifafanua kuwa hata baada ya tukio hilo, Ahmed aliripoti Polisi kama taratibu zinavyopasa, kwamba baada ya kutumia silaha, lazima taarifa zitolewe Polisi ikiwa ni pamoja na kueleza idadi ya risasi zilizotumika.
Chenge alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, alisema hawezi kulizungumzia, bali Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kufanya hivyo, kwa kuwa tukio hilo limesharipotiwa huko.
No comments:
Post a Comment