CCM Inatengeneza Wapinzani Wake Yenyewe - LEKULE

Breaking

26 Apr 2015

CCM Inatengeneza Wapinzani Wake Yenyewe



Hawra Shamte – Mwandishi wa Makala hii
Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema: “Hakuna vyama vya upinzani vyenye uwezo wa kuing’oa CCM madarakani, upinzani wa kweli utatoka CCM, wenyewe kwa wenyewe watatofautiana kisha wataanzisha chama chao.”

Ipo siku utabiri huo utatimia, utatimia kwa namna gani, mimi sifahamu. Wapo waliojaribu kutoka CCM na kuanzisha vyama vyao au kujiunga na vyama vingine vya siasa vilivyopo, pengine mshindo wao haukuweza kuing’oa CCM, lakini ni makosa tukisema kuwa mshindo wao ulikuwa mdogo.

Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa mwanachama nguli wa CCM, alipoondoka huko alijiunga na CUF. Kusema kweli CUF ilipata nguvu kisiasa Maalim Seif alipojiunga nayo. Mpaka leo CUF si chama cha kukidharau hata kidogo, kwani huko Zanzibar kinaiendesha CCM mchakamchaka.

Dk Willibroad Slaa naye alikuwa CCM, alipoondoka huko alijiunga Chadema. Nguvu za Dk Slaa Chadema si za kuzibeza hata kidogo, hivi sasa Chadema ni chama mbadala wa CCM kwa Tanzania Bara.

Vijana wengi wanajiunga na Chadema au wanakipenda chama hicho kwa sababu kwa sasa kinawapa matumaini, viongozi wake wanazungumza lugha yao. Wanaonekana kama kimbilio au mkombozi, ndiyo maana Chadema inaichachafya CCM katika maeneo mengi ya miji.

CCM nao wana kadhia zao za ndani. Unapokuwa na mawazo tofauti na wao, wanakuona kama si mwenzao, hivyo wanakufurusha. Walifanya hivyo kwa Mansour Yussuf Himid na sasa wamefanya hivyo kwa Mzee Hassan Nassor Moyo.

Pengine hawajafanya makosa kwa sababu “ndege wenye mbawa zinazofanana huruka pamoja,” sasa wewe ukiwa mbawa zako zina rangi tofauti na zao, vipi utaruka pamoja nao?

Bila shaka watakufurusha tu, kwa sababu si mwenzao, nao wana namna zao za kujilinda wasiingiliwe na maadui, hivyo wanamtilia shaka kila mwenye rangi tofauti na yao.

Hiyo ndiyo silika ya kimaumbile, na hata vyama vya siasa navyo vina silika kama hiyo, ukiwa mwanachama lazima ujenge uaminifu kwa chama na ujenge kukubalika, ukikosa sifa hizo, lazima wakushughulikie, au ukiwa kigeugeu usiyetambulika kama ni ndege au mnyama pia watakutilia shaka na hatimaye kukuengua, ili wao waendelee kubaki salama.

Lakini kwa misimamo waliyoionyesha Mansour na Moyo, yao haikuwa misimamo ya upinzani bali ilikuwa misimamo ya uzalendo kwa nchi yao.

Mwanzoni hasa wakati wa awamu ya Rais Mstaafu, Amani Abeid Karume, Wazanzibari walikuwa wamoja katika kuilinda nchi yao, kwamba Zanzibar ni nchi na kwamba wanataka iwe na mamlaka kamili.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuudadavua muungano uliopo, si kama hawautaki, la hasha, lakini wanataka muundo wake uangaliwe na ikibidi urekebishwe.

Kwao wao muungano wa serikali tatu ndiyo aula, kwani huo ndiyo wenye maslahi kwa nchi zote, Tanganyika na Zanzibar. Kwani Tanganyika itaonekana na kujitoa ndani ya koti la muungano ilimojificha na Zanzibar itakuwa na mamlaka yake ya kuamua nani wa kushirikiana naye nje ya muungano.

Mathalan suala la OIC bado linaiuma roho Zanzibar, kwani ilikatazwa kujiunga na umoja huo kwa hoja kwamba inayopaswa kujiunga ni Tanzania kwa ujumla wake.

IliambiwaTanzania ikiona kama itapata maslahi kwa kujiunga na umoja huo bila kuathiri imani za watu wake, itafanya hivyo, kwa bahati mbaya mpaka leo Tanzania haijaona umuhimu wa kujiunga na umoja huo.

Yapo pia masuala ya mgawanyo wa rasilimali za muungano na mapato ya Zanzibar, hadi leo suala hilo bado halijakaa sawa. Kimsingi Zanzibar inajiona kama ni samaki mdogo aliyemezwa na mkubwa.

Hisia hizo ndizo walizonazo takriban Wazanzibari wote, wawe CCM au CUF, lakini inafika wakati inabidi wale wa chama tawala wazidhibiti hisia hizo, kwa sababu huo si msimamo wa chama chao.

Na kwa kuwa wanahitaji kuruka pamoja, ndege wenye mbawa za aina moja, ni lazima kila mtu ahakikishe kuwa mbawa zake hazibadiliki rangi.

Hilo limeshindikana kwa Mansour na Moyo, wao walionyesha misimamo iliyopingana na ile ya chama chao, ingawa pengine ndiyo misimamo ya Wazanzibari.

Kinachoonekana kwa sasa ni kuwa CCM inaendelea kujimega kidogo kidogo hasa kwa upande wa Zanzibar. Miongoni mwa misingi yake mikuu CCM ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Binafsi nadhani anayefikiria kuuvunja Muungano akili yake ina mushkeli, huu ni wakati wa kila mtu kufikiria kuuimarisha Muungano wetu, ila sidhani kwamba fikra ya kuwa na muundo wa muungano wa Serikali tatu ni dhambi.

Ingawa msimamo kama huo ndiyo uliomsababishia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kuachishwa kazi.

CCM itaendelea kuziondoa chuya katika mchele, lakini itambue kuwa chuya zikiwa nyingi huweza kutwangwa na kuwa mchele kwani kimsingi chuya ni mpunga.

Mansour, Mzee Moyo na wengine wengi waliotoka CCM kwa sababu moja au nyingine ni chuya zinazoweza kuwa mpunga na hatimaye kutwangwa kuwa mchele.

Kwa msingi huo, CCM ijiangalie vizuri, kwani ikibidi kuwa kila unayetofautiana naye kimawazo unamtimua, chama hicho kitaganda, kwa sababu kwa kawaida maendeleo katika jambo lolote hupatikana kutokana na misigano ya kimawazo.

No comments: