Bidhaa za magendo zaipatia TRA mil 258/- - LEKULE

Breaking

11 Apr 2015

Bidhaa za magendo zaipatia TRA mil 258/-



Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kodi na faini ya jumla ya Sh milioni 258.5 kutokana na bidhaa mbalimbali za magendo zilizokamatwa katika kipindi cha Februari na Machi mwaka huu.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi huduma na elimu kwa mlipa kodi Richard Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema bidhaa hizo zilikamatwa katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera na Arusha katika operesheni inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya TRA na Jeshi la polisi kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia ya magendo nchini.

Aliongeza kuwa katika Mkoa wa Kagera, TRA imekusanya sh milioni 120.4 kutokana na kukamata katoni 2,043 za pombe aina ya Signature Vodka kutoka Uganda ambazo ni sawa na lita 24,516 yenye thamani ya sh milioni 61.9 zilizokuwa katika Jahazi ya MV Tabasamu TMZ 0541.

Kodi ya Sh milioni 66.7 ilipatikana baada ya madumu 1,599 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh milioni 65.9 kukamatwa Morogoro na kulipa kodi pamoja na faini.

Pia alisema katika Mkoa wa Tanga madumu 888 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh milioni 15.3 yalikamatwa eneo la Kwame katika bandari bubu wilayani Mkinga.

Alisema kwa kutumia taarifa kutoka kwa msamaria mwema jumla ya lita 2,290 za mafuta ya taa yenye thamani ya sh milioni 2.7 yalikamatwa mkoani Arusha yakiwa yamepakiwa katika gari aina ya Toyota Hiace yakisafirishwa kutoka Holili kwenda Moshi kwa magendo.

Katika hatua nyingine, TRA mkoani Mwanza ilikamata jahazi lijulikanalo kama MV Kalebezo ikiwa na lita 50,000 za mafuta ya taa kutoka Kenya ambayo yameingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria.

No comments: