NYOTA wa muziki na filamu Bongo, Baby Joseph Madaha amesema kuwa anatamani kuolewa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Zuber Kabwe, akisema ni mwanaume mwenye sifa zote za kuwa mume kwa mwanamke anayejiamini.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti la Risasi wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Baby Madaha ambaye alizungumzia masuala mbalimbali ya sanaa na kijamii, alisema Zitto ni mwanasiasa anayejiamini anayejua kusimamia hoja zake, hivyo kumpata mtu wa namna hiyo, ni kitu anachokitamani kitokee.
“Nafikiri Zitto ni mwanaume anayenivutia sana ambaye ningetamani anioe, licha ya kujiamini kwake, pia ana akili na ujasiri wa hali ya juu, kitu ambacho wengi hawana.
"Ukiangalia mambo ambayo ameyafanya akiwa bungeni, yanaonyesha ni jinsi gani yeye ni mtu jasiri ambaye yupo tayari kufa kwa kupigania anachokiamini,” alisema Baby.
Kuonyesha kuwa anamfuatilia mwanasiasa huyo kijana, aliorodhesha mambo kadhaa yaliyosimamiwa na Zitto bungeni bila kuogopa, la mwisho kabisa likiwa ni sakata la upotevu wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo liliishia kwa wanasiasa kadhaa kupoteza nyadhifa zao, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Licha ya kumpenda Zitto, Baby Madaha pia alisema anahusudu kujiunga na jamii ya Freemason, akisema anavutiwa na jinsi wanavyojitoa katika kusaidia watu wa jamii mbalimbali, tofauti na imani ya wengi kuwa watu hao ni wabaya.
Alitoa kauli hiyo kufuatia swali lililomuuliza imani yake kwa mambo ya kishirikina, tabia inayosemwa kufanywa na baadhi ya waigizaji na wanamuziki hapa nchini.
“Ukiniambia Freemason kweli, uchawi? Napenda Freemason maana iko wazi na kiongozi wake anajulikana, tofauti na imani za giza ambazo wahusika hawaonekani, achilia mbali kuwa wengi wao ni wachafu na wenye maisha ya shida.
“Muangalie mtu kama Chande (Alex, Kiongozi wa Freemason Tanzania) ni mtu mwenye maisha mazuri na yupo watu wanamuona, anaendesha taasisi kwa uwazi, haijalishi wako vipi, mimi ninawaelewa na ninawakubali,” alisema msanii huyo na alipoulizwa kuhusu usiri wa baadhi ya masharti ya kujiunga kama yana ishara mbaya, aliongeza;
“Siyo kila kitu mtu ajue, lazima yawepo baadhi ya mambo mnayojua wenyewe tu, angalia hata shoo ya Diamond, ameweka kiingilio kikubwa kwa sababu siyo kila mtu lazima aingie, wengine wa oyaoya waishie hukuhuku, huko kuna wenyewe, binafsi nitafurahi sana nikipata chansi, hao waliomo humo mbona hatuoni watoto wao wamekufa au wazazi wao?,” alisema kwa kuhoji Baby.
No comments:
Post a Comment