Wiki ya ‘kutafuta maji’ yaanza - LEKULE

Breaking

16 Mar 2015

Wiki ya ‘kutafuta maji’ yaanza

Dar/Mikoani. Taifa leo linaanza maadhimisho ya Wiki ya Maji, lakini vilio vimetawala kila kona ya nchi kutokana na uhaba mkubwa wa huduma hiyo muhimu kwa afya na kufanya maashimisho hayo yaoneane kuwa ni ya kutafuta maji.
Wiki ya Maji huadhimishwa kila mwaka kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kujadili kero ya huduma hiyo ya msingi na kuzindua miradi mingi, na mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa wilayani Musoma, ambako mradi wa maji ya Ziwa Victoria bado haujawa na ufanisi mkubwa.
Uhaba wa maji umekuwa kero sugu na ya muda mrefu kwa wananchi katika mikoa mingi, hasa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Mara na Tanga na Kilimanjaro, mikoa ambayo idadi yake ya watu ni zaidi ya robo ya idadi ya watu nchini kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012, na juhudi za kukabiliana na tatizo hilo hazijazaa matunda.
Ongezeko la tatizo la maji linachangiwa na ukuaji wa shughuli za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali, hususan ni kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji umeme, viwandani, utalii, uchimbaji madini, ufugaji, uvuvi na hali kadhali ongezeko la idadi ya watu.
Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya maji, shughuli za binadamu zinachangia kuharibiwa kwa vyanzo vya maji, ubovu wa miundombinu ya kusambaza maji, bajeti ndogo isiyokidhi mahitaji ya wizara husika na mipango mibovu ya kushughulikia tatizo hilo.
Dira ya taifa ya Maendeleo 2015, Mpango wa Maendeleo ya Milenia 2015 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta), sambamba na Programu ya Maendeleo ya Sekta iliyoanza mwaka 2007/08 ni mikakati inayolenga kufikisha maji kwa asilimia 100 kwa wakazi waishio mijini na asilimia 90 vijijini.
Wakati takwimu za Serikali zikionyesha kuwa asilimia 58.6 ya watu waishio vijijini wanapata maji salama na asilimia 86 ya watu waishio mijini wanapata maji safi, idadi ya watu waishio vijijini ni asilimia 80, kitu kinachoonyesha kuwa tatizo hilo bado ni kubwa.
“Mimi nafanya biashara saa zote, hata maji ya Mchina (ya bomba yaliyotandazwa na Wachina) yakitoka, bado nitapata tenda ya kuwapelekea wale wasioweza kubeba ndoo kichwani,” alisema Hamisi China, mkazi wa Tabata anayejinufaisha na tatizo hilo kwa kuuza maji.
Wafanyabiashara hao wana uwezo wa kupata kiasi cha angalau kati ya Sh5,000 hadi 10,000 kwa siku.
Maeneo ya Mbezi Kimara kuna uhaba wa maji wa kudumu na wakazi wa maeneo hayo hulazimika kununua maji yanayosambazwa kwa kutumia malori licha ya bomba la maji kutoka Ruvu kupita maeneo yao.
Wakazi hao hununua boza la lita 10,000 za maji kwa Sh75, 000, wakati kwenye maeneo mengine maji hupatikana kwa Sh250 hadi Sh500 kwa dumu moja la lita 20, kama maeneo ya Tabata.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wamesema Wiki ya Maji haina maana yoyote kwao, na wengine wamesema ingeitwa Wiki ya Uhaba wa Maji au kupendekeza fedha zinazotumika kwenye maadhimisho hayo zitumike kuchimba visima.

Biashara ya maji
Licha ya uhaba wa maji kuwatesa wananchi walio wengi, hasa akina mama, kwa upande mwingine umewafanya vijana wachache kupata ajira kwa kuuza maji.
Biashara hiyo imewanufaisha pia wafanyabiashara wenye magari ya kusambaza maji, waliojenga visima na wakati mwingine hata Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kutumia tatizo hilo kuuza maji kwa kutumia magari badala ya kutandaza mabomba ili huduma hiyo iwafikie wananchi kirahisi kwa unafuu.


Ahadi za maji
Mbali na ilani ya CCM ya 2010 -2015 iliyoahidi kuwapatia maji watu wa mijini kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia 65 ambayo haijatekelezwa, hata ahadi za viongozi mbalimbali kuhusu tatizo hilo hazijatimia.
Januari 2013 Rais Jakaya Kikwete alipokagua hali ya maji jijini Dar es Salaam, aliahidi kuwa angeitisha kikao cha wadau Ikulu kujadili suala hilo, lakini hadi sasa hajatekeleza ahadi hiyo.
Agosti 2014, Waziri wa Maji, Profesas Jumanne Maghembe alimweleza Rais Kikwete kuwa kuna miradi 1,055 inayojengwa nchini, kati ya hiyo miradi 250 imekamilika na inatoa huduma kwa watu 2,000 nchini.
Alisema miradi mingine 538 inaendelea kujengwa katika vijiji 540 na ingekuwa imekamilika ndani ya miezi sita na kuwahudumia wananchi 4,000 na miradi mingine 525 ilikuwa inafanyiwa maandalizi ya ujenzi na ingeanza kujengwa kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Mwachi 2015 lakini haijakamilika.

Kauli ya Serikali
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Amos Makalla alisema chimbuko lake ni uzalishaji mdogo wa maji ukilinganisha na mahitaji ya wakazi wa Dar es Salaam, ambao idadi yao kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012 ni milioni 4.4.
“Nafahamu tuna changamoto ya upatikanaji wa maji katika jiji letu lakini ukweli ni kwamba uzalishaji ni mdogo. Hivi sasa tunazalisha lita milioni 300 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam wakati mahitaji ni lita milioni 450 kwa siku, na kufanya upungufu wa lita milioni 150,” alisema Makalla ambaye wiki iliyopita aliahidi kuifumua Dawasco ili kupunguza ukubwa wa tatizo.
Makala alisema Serikali inatarajia tatizo kupungua baada ya kukamilika kwa miradi mitatu ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Ruvu Mpiji.
“Tunatarajia miradi hiyo itakamilika ndani ya mwaka huu... tena mmoja ulikuwa ukamilike mapema lakini kutokana na sababu mbalimbali haukuwezekana. Hivyo itakapokamilika yote tutazalisha lita milioni 700 za maji kwa siku, kiasi ambacho ni zaidi ya kile kinachohitajika,” alisema.
Akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora mwaka 2010, Rais Kikwete aliahidi kuwa wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji kutoka Ziwa Victoria na hadi sasa ahadi hiyo haijatimia.
Machi 5, mwaka huu Waziri Maghembe aliwaeleza wanahabari kuwa mradi huo umeanza na utakamilika ndani ya miezi 30 kwa gharama ya Dola 268.35 milioni za Marekani.

Uhaba wa maji na afya 
Mei 2014, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya utafiti kwa kushirikiana na taasisi 14 duniani na kubaini kuwa vifo 842,000 vilivyotokana na kuhara na kipindupindu mwaka 2014,vilisababishwa na uhaba wa maji. Hii ni sawa na asilimia 1.5 ya vifo vitokanavyo na magonjwa.
Katika ripoti maalumu iliyofanywa wilayani Handeni na gazeti hili mwaka 2010, ilionekana kuwa uhaba wa maji umekuwa chanzo cha matokeo mabaya kwa shule za wilayani humo.

No comments: