Dar es Salaam. Siku moja baada ya katibu mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa kuwataka Watanzania wajiandae kwa “Serikali Mpya”
aliyodai itapatikana Oktoba 31 baada ya Uchaguzi Mkuu, gazeti la
Mwananchi limebaini mkakati wa ushindi unaopangwa na chama hicho cha
upinzani.
Hadi sasa, Chadema ndio chama kinachoongoza
kwa upande wa upinzani kulingana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita na
wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, na inaonekana
kujipanga kupaka mafanikio makubwa zaidi mwezi Oktoba.
Katika
Uchaguzi Mkuu wa 2010, mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alishinda kwa
kupata asilimia 61.17, ikiwa ni pungufu ya asilimia 20 ya kura alizopata
mwaka 2005, wakati Chadema ilimsimamisha Dk Willbroad Slaa aliyepata
asilimia 26.34 akiwa anasimama kwa mara ya kwanza.
Huku
CCM ikiwa katika mchakato mgumu wa kumpata mrithi wa Kikwete
uliogubikwa na adhabu dhidi ya makada wanaotajwa kutaka nafasi hiyo,
Chadema iliweka mkakati wake katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika
Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari ambazo
Mwananchi imezipata, chama hicho kimelenga pamoja na mambo mengine
kupeleka madaraka kwenye ngazi ya kanda badala ya mambo yote kutegemewa
yafanywe na makao makuu.
Chadema, habari hizo zinasema,
imeunda kanda 10 ambazo ni Kanda ya Serengeti, inayoundwa na mikoa ya
Simiyu, Shinyanga na Mara, Ziwa Victoria (Geita, Mwanza, Kagera), Nyanda
za Juu Kusini (Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Iringa), Kanda ya Kusini
(Lindi na Mtwara).
Nyingine ni Kanda ya Kati (Singida,
Dodoma na Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na
Manyara), Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Kanda ya Pwani
(Temeke, Ilala na Kinondoni), Kanda ya Unguja(Kusini Unguja, Kaskazini
Unguja na Mjini ) na Kanda ya Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba).
Kanda
hizo zitawezeshwa kwa mafunzo na kiuchumi ili kuzijengea uwezo wa
kushughulikia mambo yake, hasa wakati wa uchaguzi bila ya kutegemea
ofisi kuu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kanda hizo pia
zinazindua vikundi vyake vya ulinzi, ambavyo kazi kubwa inaonekana
itakuwa ya kulinda kura ili kukabiliana na tatizo kubwa la upungufu wa
rasilimali watu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Pia kuundwa
kwa Mabaraza ya Uongozi ya Kanda kutawezesha mashauri mengi kwenye ngazi
ya mikoa kutatuliwa bila ya kutegemea ofisi kuu.
Tayari
mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameshafanya ziara kwenye
baadhi ya kanda na kufanya vikao na Mabaraza ya Uongozi ya Kanda
kuyashirikisha mikakati hiyo, sambamba na kuzindua vikundi vya ulinzi.
Lakini alipoulizwa kuhusu mpango huo, Mbowe hakutaka kuwa bayana.
“Sasa
nikiweka wazi mikakati yetu, si itakuwa kama nimewauzia wengine. Hapana
siwezi kuiweka wazi ila tunajipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema
Mbowe, ambaye pia aligombea urais mwaka 2005 wakati Kikwete akiingia
Ikulu kwa mara ya kwanza.
Lakini mtu aliye karibu na uongozi huo wa Chadema alikiri kuwapo kwa mkakati huo.
“Unajua
mkakati huo unakwenda sambamba na kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali
wa chama kuanzia ngazi ya chini kabisa,” alisema akiomba jina lake
lisitiriwe.
“Tunataka kanda hizi ziwe na uwezo wa
kupambana na si kusubiri kila jambo kutoka makao makuu.” Taarifa zaidi
zinaeleza kuwa ziara hizo za Mbowe pia zinalenga kufanya maboresho ya
kiutendaji ikiwa ni pamoja na viongozi wa chama hicho kupewa mafunzo
maalum na mbinu mbalimbali. “Chama kimebaini kuwa ili kushinda, hakiwezi
kupambana na adui kutoka sehemu moja tu, ni lazima kiwe nchi nzima.
Hilo
tumeliona katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema mtoaji habari
huyo. “Kinachofanywa sasa ni kuhakikisha kuwa kila kanda inakuwa na
nguvu ya kufanya mambo yake yenyewe.
Yaani kila kanda
itaweka mkakati wake wa kukiimarisha chama na kukabiliana na misukosuko
yote ya kisiasa. Makao makuu ya chama yatakuwa yakitoa maelekezo tu.”
Jumamosi iliyopita, Dk Slaa alisema katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Isaka wilayani Kahama kuwa nchi haina budi kujiandaa kwa
serikali mpya.
Alisema Chadema itashika nchi kwa kuwa
wananchi wamechoshwa na serikali iliyopo sasa ya CCM, kwamba ili
kuongeza nguvu za kuking’oa chama hicho kikongwe, wananchi wanapaswa
kuunga mkono juhudi za Ukawa.
Dk Slaa, ambaye aliwahi
kuwa mbunge wa Karatu kabla ya kugombea urais mwaka 2010, anatazamiwa
kuteuliwa tena na chama chake kuwania urais na ni mmoja wa watu
wanaopewa nafasi kubwa ya kupitishwa na Ukawa kupeperusha bendera ya
upinzani dhidi ya mgombea wa CCM, kwenye mbio za Ikulu.
Mbali
na kufanya vizuri mwaka 2010, Chadema ilipiga hatua kubwa zaidi kwenye
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana baada
ya kunyakua viti vingi vilivyokuwa vinashikiliwa na CCM na vyama vingine
vya upinzani.
Chadema ilifanya vyema zaidi katika
Kanda ya Serengeti kwa kupata kura nyingi katika vijiji, vitongoji na
mitaa, kura ambazo hazijafikiwa na kanda yoyote.
Kanda nyingine zilizofuatia kwa kufanya vizuri katika uchaguzi huo ni Kanda ya Ziwa Victoria na Kanda za Kaskazini.
No comments:
Post a Comment