WATEJA WA VODACOM M-PESA SASA KUTUMA PESA NCHINI KENYA - LEKULE

Breaking

9 Mar 2015

WATEJA WA VODACOM M-PESA SASA KUTUMA PESA NCHINI KENYA


Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa kutuma na kupokea pesa nchini Kenya kwa njia ya M-PESA. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania, Bernard Dadi (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Maendeleo ya M-Pesa wa Vodacom Tanzania, Isack Nchunda wakimsikiliza jambo Meneja wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu Tanzania, James Masoy (katikati) wakati wa uzinduzi wa kutuma na kupokea pesa nchini Kenya kwa njia ya M-PESA. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania, Bernard Dadi (katikati) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza (kushoto) baada ya uzinduzi rasmi wa kutuma na kupokea pesa nchini Kenya kwa njia ya M-PESA uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu Tanzania, James Masoy.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza (kulia) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania, Bernard Dadi (katikati) na Meneja wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu Tanzania, James Masoy, mara baada ya uzinduzi rasmi wa kutuma na kupokea pesa nchini Kenya kwa njia ya M-PESA uliofanyika jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam, Tanzania, Machi 9,2015: Kampuni kubwa za mawasiliano Afrika mashariki Vodacom Tanzania na Safaricom ya Kenya leo zimezindua huduma mpya ambapo kuanzia sasa zaidi ya wateja Milioni 7 wa M-Pesa waVodacom Tanzania wanaweza kutuma na kupokea pesa kwa watumiaji zaidi ya milioni 18 wa Safaricom M-Pesa ya Kenya. Huduma hii mpya ambayo imebuniwa na makampuni haya yanayoongoza kutoka huduma za mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki itawawezesha wateja wake kutuma pesa kwa kutozwa viwango sawa na vinavyotumika katika nchi husika.

Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hii,Mkurugenzi

Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza alisema kuwa takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2013 zaidi ya shilingi bilioni 200 zilitumwa kutoka Tanzania kwenda Kenya halikadhalika zaidi ya bilioni 1 zilitumwa kutoka Kenya kuja Tanzania. “Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa fedha karibu shilingi bilioni 200 zilizotumwa nchi Kenya kutoka Tanzania zilitumwa kwa njia rasmi za utumaji fedha na inakadiriwa kuwa kiasi cha fedha hizo zaidi ya mara mbili zimetumwa kwa njia zisizo rasmi za utumaji fedha ikiwemo kutumia madereva na makondakta wa mabasi au kutumia ndugu na marafiki wanaosafiri”amesema Meza.

“Tumeona ugumu wanaokabiliana nao wateja wetu kutuma fedha katika nchi jirani ya Kenya na tumepata suluhisho kwa kuleta huduma hii ambayo ni ya haraka na uhakika.Kuanzia leo hakuna sababu ya kutuma pesa kwa kumtumia dereva au kondakta wa basi au kutozwa gharama kubwa kutoka taasisi za kifedha unapolipa karo za watoto wanaosoma nchini humo,unaweza sasa kufanya malipo na kulipa ankkra mbalimbali kutoka pochi ya M-Pesa ukiwa umetulia nyumbani kwako,”amesema Meza.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Safaricom Bob Collymore alisema “Tunaamini tumefungua ukurasa mpya wa kuendeleza huduma ya M-Pesa kwa kuwezesha wateja wa Kenya na Tanzania kutumia huduma hii katika kutumiana fedha na kufanya malipo katika nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya”.Alisema

Alisema katika awamu hii ya kwanza iliyozinduliwa leo inawawezesha wateja kutuma pesa Kenya kama ambavyo wamekuwa wakituma hapa nchini, tofauti itakuwa wakati wa kutuma pesa kwenye simu kutakuwepo na kipengele kinachoonyesha kuwa wanataka kutuma pesa kwa M-Pesa ya Kenya na kuandika namba za mpokeaji kwa kutumia namba za Kenya yaani +254 na katika awamu ya pili ya huduma hii wateja wa Safaricom ya Kenya wataweza kutuma pesa kwa wateja wa Vodacom Tanzania kupitia huduma hii.”

No comments: