Wananchi Toka Mara Waandamana Kwenda Monduli Kwa Lowassa.......Wamkosa na Kuacha Ujumbe Mzito Kwa CCM - LEKULE

Breaking

30 Mar 2015

Wananchi Toka Mara Waandamana Kwenda Monduli Kwa Lowassa.......Wamkosa na Kuacha Ujumbe Mzito Kwa CCM



WANANCHI wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamekitaka Chama Cha Mapiduzi (CCM) kutokuzuia demokrasia ya wanachama kushawishi wagombea wa Urais wanaoona kuwa wanafaa kuwatetea kiti hicho.

Wakizungumza juzi baada ya kufika nyumbani kwake kwa lengo la kumshawishi Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kugombea nafasi ya Urais, wananchi hao walisema kuwa ni vyema chama kikawaacha wapenzi na mashabiki wa Lowassa kuendelea kumshawishi agombee na nafasi hiyo.

Aliyekuwa katibu wa umoja wa wanawake wa (UWT) CCM wilaya ya Serengeti, Anna Mathayo Chacha alisema kuwa Lowasa ndiye chaguo lao kwa kuwa ni kiongozi wanayeamini kuwa ataivusha nchi kutoka hapa ilipo ikiwa ni pamoja na kukipa heshima na nguvu Chama.

Aidha alisema kuwa wananchi wanahitaji utawala bora kwa sasa na mtu pekee ambaye wanadhani anatosha nafasi hiyo ni Edward Lowasa kwa kuwa ni kiongozi mwenye maamuzi magumu ambaye anaweza kusimamia utawala bora hivyo viongozi wa ngazi za juu wasizue demeokrasia ya wananchi kusema ambacho wanahisi ni sahihi kwao.

Diwani wa kata ya Ikoma, Sebastian Sabasaba Banagi alisema kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu hivyo kitendo cha kuzuiwa kwa wananchi kueleza hisia zao siyo jambo la kidemokrasia bali linakandamiza uhuru wa kusema wanachokiamini.

Alisema kuwa suluhu ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu ni kumpitisha Lowasa kwa kuwa wao kama viongozi ambao wanawawakilisha wananchi, wananchi wanampendekeza kiongozi huyo kuwania kiti hcho kutokana na matumaini na imani kubwa walioyo nayo kwake.

“Kama alivyosema Waziri mkuu mstaafu, Lowasa kuwa huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono ni sahihi kabisa hata sisi tunaliunga mkono hilo hakuna mtu yeyote anayeweza kuzuia hisia za watu juu ya kiongozi huyu mahiri,” alisema Banagi

Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM wilaya ya Serengeti, Daniel Kegocha aliomba Chama hicho kuona umuhimu wa kupitisha jina la mgombea huyo kwa kuwa ni chaguo la walio wengi na yeyote anayetokea kupinga atakuwa ni msaliti katika chama hicho.

Alisema kuwa, ni vizuri kamati kuu ya Chama ikae kwa pamoja itafakari na kuona umuhimu mkubwa wa kumpitisha mgombea huyo kwa kuwa kila kona ya nchi wana imani naye na wana amini atawaletea maendeleo na kuliunganisha Taifa.

Wananchi hao kutoka wilayani Serengeti wakiongozwa na Madiwani na waliowahi kushika nyadhifa katika chama hicho wapatao 65, walifika wilayani Monduli ili kumshawishi Mbunge huyo kutokata tamaa na kuendelea na nia ya kuchukua fomu huku wakiahidi kuwa watamfuata alipo ili kumshawishi na kuzungumza naye.

No comments: